MAKALA: Huyu ndiye mwanasoka tajiri zaidi duniani

FAIQ BOLKIAH

Muktasari:

>> Faiq Bolkiah ni mpwa wa Sultan wa Brunei, Hassanal Bolkiah, ambaye utajiri wake unakadiriwa kuwa Dola 20 milioni.

LEICESTER,  ENGLAND

MARA Paap! Ukiambiwa utaje wanasoka matajiri duniani, basi moja kwa moja utaanza kutaja Cristiano Ronaldo, Lionel Messi na Neymar.

Hutothubutu kulitaja jina la kinda wa miaka 19 tu, tena anayecheza kwenye kikosi cha rizevu huko Leicester City, Faiq Bolkiah.

Kwa taarifa yako, kinda huyo ndiye mwanasoka tajiri zaidi duniani. Anacheza mpira kujifurahisha tu na si kutaka ile mishahara mikubwa ya kila wiki, ambayo Ronaldo na Messi mara kwa mara wamekuwa wakizisumbua klabu zao ziwalipe.

Faiq Bolkiah ni mpwa wa Sultan wa Brunei, Hassanal Bolkiah, ambaye utajiri wake unakadiriwa kuwa Dola 20 milioni.

Bolkiah Jr ni winga kwenye kipaji cha hali ya juu sana akiichezea Leicester City na yupo England kwa muda mrefu sasa baada ya kuanzia soka lake huko AFC Newbury, akiwa mtoto zaidi.

Mwaka 2009, Southampton ilimchukua Bolkiah na kumwongeza kwenye akademia yao. Hawakuwa wamempa mkataba. Mwaka 2013, Arsenal ilimwita kumfanyia majaribio katika kikosi chao.

Bolkiah aliichezea Arsenal katika mashindano ya Kombe la Lion City na alifunga bao kwenye michuano hiyo iliyofanyika mwaka 2013. Baada ya kuona kipaji chake, Chelsea ilimnasa juu kwa juu na kumsainisha mkataba wa miaka miwili. Lakini, baada ya mwaka mmoja tu, Bolkiah aliachana na Chelsea na kwenda kujiunga na Leicester City, iliyomsainisha mkataba wa miaka mitatu.

Licha ya alizaliwa Los Angeles, Marekani, Bolkiah alichagua kuichezea Brunei katika soka la kimataifa na ameiwakilisha nchi hiyo mara tisa na kufunga bao moja.

Kwa kukumegea tu ukweli kuhusu utajiri wa winga huyo, basi tazama utajiri wa baba yake, anayeitwa Jefri. Jefri ni kaka wa Sultan wa Brunei, ambaye ameripotiwa kutumia Pauni 10 bilioni ndani ya miaka 15 na ndiye Mkurugenzi wa Brunei Investment Agency.

Kuna wakati, Jefri alitumia Pauni 35 milioni ndani ya mwezi mmoja kwa ajili ya kununua magari, saa pamoja na peni ya dhahabu nyeupe.

Baba wa winga huyo wa Leciester City anaaminika pia kumiliki magari yapatayo 2,300, yakiwamo ya kifahari kama Bentley, Ferrari na Rolls-Royce.

Kitu cha kuvutia zaidi, wakati Jefri alipokuwa akisherehekea kutimiza umri wa miaka 50, alimsafirisha Michael Jackson kwenda kufanya shoo kwenye sherehe yake binafsi. Ndiyo, Michael Jackson huyu anayemfahamu wewe ambaye kwa sasa ni marehemu alichukuliwa kwenye kumburudisha tajiri huyo wa Brunei, ambaye ndiye baba yake Bolkiah.

Kwenye sherehe hiyo alijenga uwanja maalumu kwa ajili ya tukio na Mfalme huyo wa Pop, alilipwa Pauni 12.5 milioni kwa ajili ya burudani aliyotoa kwenye sherehe hiyo. Kwa utajiri huo utashangaa kwa nini, Faiq Bolkiah anacheza mpira kutoka jasho tu uwanjani.

Katika mahojiano yake, ambapo mara chache sana amekuwa akizungumza, winga huyo wa Leicester City, alisema: “Nimekuwa nikicheza mpira tangu nikiwa mdogo sana na nimekuwa nikifurahia kutembea nikiwa na mpira kwenye miguu yangu.

“Wazazi wangu siku zote wamekuwa wakinisapoti kutimiza ndoto zangu za kuwa mwanasoka. Wamekuwa wakinisaidia kufanya mazoezini ya kisaikolojia na kimwili tangu utotoni mwangu, hivyo wao ndiyo mashujaa wangu.”