Hawawekwi benchi kizembe PALE Man City

MANCHESTER, ENGLAND. PEP Guardiola ametikiswa na kutema taji moja kutokana na kutupwa nje ya michuano ya Kombe la FA kwa kupigwa 1-0 na Wigan Athletic Jumatatu iliyopita. Kipigo hicho kinapunguza idadi ya mataji iliyokuwa ikifukuzia Manchester City kwa msimu huu na sasa kubaki kwenye michuano mitatu tu, Ligi Kuu England, Ligi ya Mabingwa Ulaya na Kombe la Ligi na watacheza fainali na Arsenal.

Kwa msimu huu, Guardiola ana mengi ya kujivunia kutoka kwa wachezaji wake, lakini zaidi na zaidi ni kuhusu mastaa waliocheza mechi nyingi za msimu huu.

Hii ndiyo orodha ya wachezaji waliocheza mechi nyingi kwenye kikosi cha Man City msimu huu.

Bernardo Silva – mechi 39, mabao 5

Staa wa Kireno, Bernardo Silva ndiye mchezaji aliyecheza mechi nyingi zaidi kwenye kikosi cha Manchester City kwa msimu huu kuliko mwingine yeyote katika kikosi hicho cha Etihad.

Kiungo huyo mshambuliaji amecheza mechi 39 na kufunga mabao matano huku akihusika pia kwenye asisti tisa.

Kevin De Bruyne – mechi 38, mabao 11

Ndiye mchezaji aliyekuwa kwenye ubora mkubwa zaidi kwa msimu huu kwenye kikosi hicho cha Man City. Asisti zake na mabao yake yamechangia pointi nyingi sana kwa timu hiyo ya Guardiola na kwa msimu huu Mbelgiji huyo amepangwa katika mechi 38, akifunga mabao 11 na kutoa asisti 19.

Fernandinho – mechi 37, mabao 3

Mchapakazi wa Man City kwa msimu huu. Mbrazili, Fernandinho huduma yake anayotoa kwenye kikosi hicho hakika ni bora na inamfanya Guardiola kuwa na wakati mzuri anapokuwa naye ndani ya uwanja.

Fernandinho amecheza mechi 37 msimu na kuhusika kwenye mabao matatu na asisti tatu.

Mchezaji mwingine aliyecheza idadi kama hiyo ya mechi ni Kyle Walker, hajafunga bao, lakini ametoa asisti sita.

Raheem Sterling –

mechi 36, mabao 20

Sterling amekuwa katika kiwango bora kabisa msimu huu na jambo hilo ndilo linalomfanya Kocha Guardiola asithubutu kabisa kumweka nje ya uwanja anapofahamu wazi mchezaji wake hana tatizo lolote.

Kwa msimu huu, Sterling ni mmoja wa wachezaji waliocheza mechi nyingi katika kikosi hicho cha Etihad akicheza mechi 36, amefunga mabao 20 na kuasisti saba.

Nicolas Otamendi – mechi 35, mabao 5

Beki wa kati, Nicolas Otamendi ni staa ambaye kiwango chake cha soka kwa msimu huu kimekuwa juu na kuwa msaada mkubwa kwenye kikosi cha Man City.

Otamendi amecheza mechi 35 za Man City msimu huu na kutoa mchango mkubwa ukiacha kwenye kuzuia timu yake isifungwe, lakini beki huyo wa kati amesaidia timu yake kupata mabao baada ya kufunga mara tano. Hana asisti, lakini kwa kile alichokifanya ni msaada mkubwa.

Leroy Sane –

mechi 34, mabao 11

Mjerumani, Leroy Sane ni moja ya silaha za nguvu kabisa kwenye kikosi cha Man City kwa msimu huu. Majeruhi yake yaliacha Man City kwenye pigo kubwa kutokana na kuikosa huduma yake muhimu.

Sane ni miongoni mwa walioitumikia Man City mara nyingi msimu huu akicheza mechi 34 na kufunga mabao 11 huku akiwa pia na asisti 14. Mchezaji mwingine aliyecheza idadi kama hiyo ya mechi ni kipa Ederson.

Sergio Aguero –

mechi 33, mabao 29

Straika, Sergio Aguero hajawahi kuwa mzigo kwenye kikosi cha Man City kutokana na huduma yake matata kabisa anayotoa kwenye kikosi hicho. Msimu huu mchango wake ni mkubwa na jambo hilo limeifanya Man City kuendelea kutesa kwenye michuano inayoshiriki hasa kutokana na mechi zake 33 alizocheza kufunga mabao 29 na kuasisti mara sita.

Aguero ambaye mwishoni mwa msimu uliopita alihusishwa na mpango wa kuondoka kwenye timu hiyo, mambo yamegeuka na kuwa mchezaji muhimu chini ya Guardiola.

Wachezaji wengine

Kwenye orodha ya waliocheza mechi nyingi kwenye kikosi cha Man City wapo pia Ilkay Gundogan, aliyecheza mechi 32, wakati David Silva amecheza mechi 28, Mbrazili Danilo amecheza mechi 27 sawa na Mbrazili mwenzake, Gabriel Jesus. John Stones amecheza mechi 25, Fabian Delph mechi 22, Eliaquim Mangala aliyetolewa kwa mkopo mwezi uliopita, yeye amecheza mechi 15, Vincent Kompany mechi 12 na Yaya Toure amecheza mechi 11.