Harmonize awarudia mashabiki wake Mtwara

Friday December 29 2017

 

By Haika Kimaro

Mtwara. Msanii wa muziki wa kizazi kipya, kutoka Familia ya Wasafi (WCB), Rajab Abdul maarufu Harmonize ametoa msaada wa fimbo nyeupe 30 kwa walemavu wa macho  mkoani Mtwara ikiwa ni mwendelezo wa kutoa misaada mbalimbali kwa makundi yenye mahitaji maalumu mkoani humo. 

Pia, jana Alhamisi msanii hiyo alikula chakula pamoja na watoto yatima katika kituo cha Kanisa EAGT alichokiandaa kwa kushirikiana na Hoteli ya Tiffany Diamond.

Akizungumza wakati  wa makabidhiano, Harmonize amesema "Katika kuelekea misimu ya kusherekea sikukuu lazima tukumbuke kuna wenzetu wana mahitaji maalumu hivyo nikaona sio vibaya kwa sababu nilipata taarifa wana uhitaji wa fimbo nyeupe kwa uwezo wangu nimeweza kuleta fimbo 30 niwaombe na wengine kuwaona ndugu zetu hawa kwa sababu wana uhitaji wa fimbo zaidi ya 100 na mahitaji mengine," amesema Harmonize.

Akizungumza katibu wa chama cha wasioona mkoani Mtwara, Ally Ismail  amesema bado wana uhitaji mkubwa na kuwaomba wadau kujitokeza zaidi.

"Msaada bado unahitajika tunaomba wafadhili wajitokeze ili kutukomboa, tutafurahi sana kama watajitokeza wafadhili na kutuanzia mradi sisi tusioone ili tuweze kujimudu katika maisha yetu ya kila siku, "amesema Ismail