Hao simba hawatanii

Muktasari:

Simba ilipata ushindi huo wa mabao 2-0 kwenye Uwanja wa Kaitaba mjini hapa na kufanikiwa kulipa kisasi cha msimu uliopita ilipolala mabao 2-1 uwanjani hapa huku bao la kiungo Said Ndemla likiwa gumzo kwa namna lilivyotengenezwa kabla.

ACHANA na bao la pili la kichwa la John Bocco ‘Adebayor’ ambalo linakuwa la kumi kwake kumtungua kipa Juma Kaseja, Simba imeonyesha wazi kuwa kweli inautaka ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu huu baada ya jana Jumatatu kuichapa Kagera Sugar.

Simba ilipata ushindi huo wa mabao 2-0 kwenye Uwanja wa Kaitaba mjini hapa na kufanikiwa kulipa kisasi cha msimu uliopita ilipolala mabao 2-1 uwanjani hapa huku bao la kiungo Said Ndemla likiwa gumzo kwa namna lilivyotengenezwa kabla.

Ushindi wa jana umeirejesha Simba kileleni mwa msimamo ikiing’oa Azam FC iliyokuwa imekaa kwa muda baada ya ushindi wake wa juzi Jumapili wa mabao 2-0 ugenini dhidi ya Prisons Mbeya.

Simba imefikisha pointi 32, alama mbili zaidi ya ilizonazo Azam huku Yanga ikiwa nafasi ya tatu kwa pointi 25 sawa na Mtibwa Sugar iliyo ya nne, huku timu zote zikiwa zimeshacheza mechi 14 kila moja.

Katika mchezo huo wa jana, katika dakika 20 za mwanzoni Kagera ilicheza kwa nidhamu ya juu na kujenga mashambulizi yake kupitia pembeni kwa Pastory Athanas na Ally Nassoro ‘Ufudu’.

Juma Nyosso na Mohammed Fakhi wa Kagera pamoja na Bocco walionyeshwa kadi za njano katika kipindi cha kwanza. Jaffar Kibaya naye alipoteza nafasi ya kuipa uongozi timu yake baada ya shuti lake kwenda nje kidogo ya lango.

Ufudu na Kibaya walipoteza pia nafasi za wazi kwa timu yao na katika dakika ya 66 Bocco alipiga shuti kali lililodakwa na Kaseja kabla ya vijana wa Simba kutengeneza bao la kwanza lililofungwa na Ndemla kwa shuti kali dakika tatu tu baadaye akiunganisha pasi murua ya Kichuya.

Bao lilivyokuwa

Bao hilo lililoacha gumzo Kaitaba, lilianzia kwa nahodha Bocco kuchomoka na mpira akiandambwa na Fakhi na kupiga krosi iliyomfikia Okwi aliyepiga pasi ya kichwa kwa Kichuya aliyekuwa amezongwa na mabeki wa Kagera kabla ya kutoa pasi murua kwa Ndemla.

Ndemla akiwa katika nafasi nzuri kama kawaida yake aliachia fataki lililoenda moja kwa moja kimiani likimuacha Kaseja akikosa la kufanya na kuamsha shangwe kwa mashabiki wa Simba waliofurika uwanjani hapo.

Wakati Kagera ikitafakari namna ya kurejesha bao hilo, Bocco alizidi kuwakatisha tamaa baada ya kutupia bao la pili kwa kichwa dakika ya 79 akiunganisha krosi tamu ya beki Shomary Kapombe aliyekuwa akicheza kwa mara ya kwanza tangu asajiliwe Simba msimu huu akitokea Azam sambamba na Bocco.

Kapombe aliyeingia kipindi cha pili akichukua nafasi ya Nicholas Gyan, alimzidi ujanja Adeyum Saleh wa Kagera kabla ya kupiga krosi hiyo iliyotua kichwani mwa Bocco na kufunga bao lake la tano msimu huu na la 10 dhidi ya Kaseja katika mechi za mashindano.

Katika kipindi hicho cha pili nahodha wa Kagera, George Kavila na Juuko wa Simba walionyesha kadi za njano kwa mchezo mbaya, huku timu zote zikifanya mabadiliko ya wachezaji Simba ikimtoa James Kotei na Kichuya ili kuwaingiza Mavugo na Mzamiru Yassin na Kagera ikiwatoa Pastory na Atupele na kuwaingiza Edward Christopher na Peter Mwalyanzi.

Nyosso amzimisha shabiki

Mara baada ya pambano hilo beki Nyosso alijikuta akibebwa na walinda usalama uwanjani hapo baada ya kumtwanga ngumi shabiki wa Simba aliyemkejeli na kumsababisha kuzimia kabla ya kukimbizwa hospitalini kwa matibabu.

Singida mambo bado

Katika pambano jingine la Ligi Kuu Bara, Singida United ikiwa ugenini mjini Songea iling’ang’aniwa na wenyeji wao Majimaji kwa kulazimishwa sare ya bao 1-1 kwenye Uwanja wa Majimaji. Wenyeji walilazimika kusubiri mpaka dakika ya 83 kuchomoa bao la kipindi cha kwanza la Singida lililotupiwa kambani na Papii Kambale katika dakika ya 23.

Bao hilo la kusawazisha la Majimaji lilifungwa na mkongwe Peter Mapunda na kuipa pointi moja muhimu Majimaji iliyowatoa nafasi ya 14 hadi ya 10 ikifikisha pointi 13, huku wapinzani wao wakisalia nafasi ya tano wakiwa na alama zao 24.