Hao Simba, sasa mwendo wa pipa tu

Tuesday February 13 2018

 

By DORIS MALIYAGA

KIKOSI cha Simba kinaondoka alfajiri ya leo Jumanne kwa ndege ya Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) kuwahi mechi yao dhidi ya Mwadui FC ya Ligi Kuu Bara itakayopigwa keshokutwa Alhamisi kabla ya Jumapili kupaa kwenda Djibouti kumalizia kazi ya kuizika Gendarmarie.

Simba iliyoichapa Gendarmarie mabao 4-0 juzi Jumapili kwenye Kombe la Shirikisho barani Afrika, itarudiana nao Jumanne ijayo, inasafiri na ndege kuifuata Mwadui ili kujikinga na uchovu kwani imepania kuzidi kutoa dozi kujichimbia zaidi kileleni ilipo sasa kwa pointi 41 dhidi ya 34 za Yanga iliyo nafasi ya pili.

Akizungumzia maandalizi ya timu yake kiufundi, Kocha Msaidizi wa Wekundu wa Msimbazi hao, Masudi Djuma, alisema timu yao ipo vizuri na wanajiweka tayari kwa ajili ya kufanya vizuri zaidi kwenye mechi zote kama ilivyopangwa.

“Tumejiandaa vizuri kuhakikisha kila kitu kinakwenda sawa, kwanza tutaanza na mchezo wa ligi maana ushindani sasa ni mkubwa,” alisema.

“Tunataka kuona tunaendelea kukusanya pointi tatu kwa mabao mengi kadiri inavyowezekana.

“Kisha tunataka kufanya hivyo pia kimataifa kama tulivyoanza. Tutapambana siku zote.”