Gor Mahia yaivaa Leones Ligi ya Mabingwa

Friday February 9 2018

 

By THOMAS MATIKO

Nairobi.KOCHA wa Gor Mahia, Dylan Kerr kasema japo hana ufahamu kuhusu wapinzani wao, Leones Vegeterionaos wa Equatorial Guinea ambao watakaopambana nao kwenye mechi ijayo Jumamosi hii kuwania kufuzu kwa CAF Champions league, lakini tayari ana dawa ya kuwaangamiza.

Kerr amekuwa mwingi wa shughuli mazoezini tangu mwanzo wa juma hili akizidisha mbinu za maandalizi kuhakikisha kikosi chake kipo vizuri kupambana na Vegeterianos, timu ambayo kasisitiza kuwa hana habari nayo kuhusu mbinu au mtindo wao wa uchezaji.

“Hii ni mechi ngumu kwetu kwa sababu hatujui cha kutarajia kutoka kwa wapinzani wetu ukizingatia kuwa, hatuna ufahamu wowote kuwahusu.

“Nimejitahidi kufanya utafiti wangu angalau kujua staili yao ya uchezaji, lakini sijafanikiwa. Tunakwenda kwenye mechi hii tukiwa kama vipofu vile ila kwa upande wao nina uhakika lazima watakuwa wamecheki baadhi ya mechi zetu hivyo, watakuwa wanatuelewa kwa kiwango fulani,” Kerr alitanguliza.

Kutokana na hali hiyo, kocha huyo kasema  ataingia kwenye mechi hiyo kwa staili yake ila  akatoboa siri ya mabadiliko atakayofanya kuhakikisha kuwa wanajilinda.

“Itanilazimu nibadilishe mfumo kidogo ila staili yetu itabakia ile ile kwa sababu tunahitaji kujilinda. Kwa maana hiyo nitaanza na walinzi watano ili kujipa muda wa kuisoma mechi itakapokuwa ikiendelea ndipo niweze kuwa na maamuzi mengine,” akaongeza.

Gor hawajawahi kufika hatua ya makundi ya dimba hilo kasumba anayolenga kuivunja Kerr msimu huu kwa kuhakikisha anaanza kwa kishindo kwa kuwalima Leones watakapovaana nao Jumamosi uwanjani Machakos kabla ya kusafiri wiki moja baadaye kwa marudiano.