Fifa yasuuzika kasi ya Rais Magufuli

Dar es Salaam. Rais John Magufuli anapambana na rushwa na hata Tanzania kupaa katika anga za kimataifa kwa kasi hiyo na hiyo imemfanya Rais wa Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa), Gianni Infantino amsifu.

Sifa za Infantino kwa Rais Magufuli ni baada ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kumweleza kuwa tangu Rais Magufuli aingie madarakani amekuwa akipambana na rushwa na ufisadi wa rasilimali sawa na vita vyake (Infantino) kupambana na rushwa katika soka.

 

Waziri Mkuu alisema Tanzania inatambua masuala ya michezo na inaunga mkono kazi nzuri ya Fifa katika kuendeleza soka duniani lakini kubwa ni mpango wake katika mapambano dhidi ya rushwa katika soka duniani.

Alisema kuwa hiyo itasaidia kueneza ujumbe kwa vyama na mashirikisho ya soka kimataifa kujisafisha kwa kupambana na rushwa hadi kufikia mafanikio.

Waziri Mkuu alisema kuwa Fifa ikifanikiwa katika mapambano hayo, itasaidia kwa kiasi kikubwa katika kuweka mazingira sawa ya soka pamoja na uwajibikaji ambao ndiyo msingi wa utawala bora.

Infantino akiwa na Ahmad Ahmad, Rais wa CAF ofisini kwa Waziri Mkuu, alimsifu Rais kwa hatua hiyo na kusema kuwa rushwa ni mbaya na ndiyo chanzo cha kurudi nyuma maendeleo ya soka duniani.

"Tafadhali, tunaomba mheshimiwa Waziri Mkuu tupelekee salamu zetu za pongezi kwa Rais kwa mapambano ya rushwa...tumefurahi kusikia Rais anapambana na rushwa na huu ndio mpango wa Fifa kupambana na rushwa katika soka duniani," alisema Infantino.

Alisema kuwa mapambano ya rushwa hayatakiwi kukoma kwa kuwa yanagusa kila eneo la michezo ikiwemo katika uwekezaji hasa wa miundombinu ya soka.

Infantino aliwataka Watanzania kuunganisha nguvu moja katika mapambano ya rushwa hasa katika soka na siku moja Tanzania itapiga hatua za mbali katika mchezo huo na pia kuwa na utawala bora.

Rais huyo wa Fifa ambaye aliingia madarakani Februari 2016, mpango wake wa kwanza kuutangaza ni kuhakikisha anapambana na rushwa  akatika soka lakini pia kuwepo na uwazi na ukweli katika mapato na matumizi.

Aliahidi kulisimamia hilo akisema kuwa uwazi ni jambo la msingi hasa katika fedha na kwamba kila senti inayoingia kwenye chama na inayotoka lazima iwe na maelezo, hapo ndipo litakamilika suala la uwazi.