Euro Nets, Lufa hapatoshi kesho

Muktasari:

Mashindano hayo yanalengo la kuibua vipaji kwa wachezaji chipukizi nchini Kenya

Nairobi. Timu ya Euro Nuts na Lufa zitamenyana kesho Jumapili katika fainali kumtafuta bingwa wa Chapa Dimba kwa upande wa wanaume.

Timu hizo zilijikatia tiketi katika mechi za hatua ya nusu fainali zilizopigwa kwenye uwanja wa Chuo cha ufundi cha Thika mapema leo.

Katika mchezo wa nusu fainali ya kwanza iliyosakatwa majira ya saa sita mchana, ilizikutanisha Euro Nets kutoka Laikipia na Juja United ya Kiambu ambapo baada ya 90, timu zote zilitoshana nguvu kwa sare ya 0-0.

Mwamuzi aliamuru matuta yapigwe ambapo Euro Nets ilishinda kwa penalti 4-3. Wafungaji wa Euro Nets walikuwa ni Riek Nhiah, Hezekiah Nyati, John Njuguna na Brian Mukena huku Eusavia Okila, Wainaina Joseph na Mwangi John wakiifungia Juja United.

Kwa upande wake, timu ya Lufa ilijikatia tiketi baada ya kuibanjua Inter City mabao 4-0, katika mechi ya nusu fainali ya pili, iliyopigwa saa tisa alasiri kwenye uwanja huo, mfungaji akiwa ni Kiloku Ronald kunako dakika ya 39.

Baada ya kupata bao hilo, Lufa waliongeza mashambulizi lkini hadi mapumziko matokeo yalikuwa ni 1-0. Kipindi cha pili kilianza kwa kasi ambapo Lufa ambao walionekana kukamia ushindi waliendelea kuvamia lango la Inter City.

Katika dakika ya 47 Inter City walipata bao lakini mwamuzi akalikataa. Dakika mbili baadae Lufa wakafanya mashambulizi yakushtukiza na kujiandikia bao la pili kupitia kwa Mwaura Erick.

Mabao mengine yalipatikana katika dakika ya 65 na 89 wafungaji wakiwa ni Gichuhi Samwel na Maraka Fredrick.