Eti Yanga ilitamani kucheza na Simba!

Thursday January 11 2018

 

HAIFAHAMIKI kama ni kweli ila ndiyo hivyo, Yanga imefichua siri kuwa ilitamani kuvaana na Simba katika mechi ya nusu fainali ama fainali ya Kombe la Mapinduzi ili tu kulipa kisasi cha mechi yao ya msimu uliopita, lakini mambo yamekwenda ndivyo sivyo kwa mahasimu wao hao.

Simba iliaga mashindano hayo katika hatua ya makundi baada ya kupokea vipigo viwili mfululizo kutoka kwa Azam na URA hivyo, kuzima ndoto ya Wanajangwani hao ambao hawakamatiki katika mashindano ya mwaka huu.

Katika mashindano ya mwaka jana Yanga na Simba zilikutana katika hatua ya nusu fainali na Wanamsimbazi hao kuibuka kidedea kwa mikwaju ya penalti.

Kocha Msaidizi wa Yanga, Shadrack Nsajigwa na hata baadhi ya nyota wa kikosi chake walisema akili zao zote walielekeza dhidi ya Simba, lakini imetokea bahati mbaya watani zao hao wakaaga mashindano hayo mapema.

Nsajigwa alisema tangu walipotua visiwani humu walijiandaa kucheza na timu yoyote katika hatua ya makundi na hata kwenye mtoano, lakini walikuwa na hamu sana ya kuumana na Simba ili kulipa kisasi chao.

“Tulikuwa tayari kupambana na timu yoyote ambayo ingekuja mbele yetu, ila tulitamani sana kukutana na Simba, lakini wametolewa na sasa tunaelekeza nguvu ili kuona mwaka huu tunarudi na kombe,” alisema Nsajigwa.