Eti, St Louis wanakufa mapema kwao

Muktasari:

  • Martin alisema uwepo kwa Juma Mahadhi, Ibrahim Ajib, Geofrey Mwashiuya, yeye na Kabamba Tshishimbi pamoja na nyota wengine wa timu yao, hawaoni chochote cha kuwazuia kuwang’oa St Louis waliolala jijini Dar es Salaam kwa bao 1-0.

YANGA imeondoka alfajiri ya leo Jumapili kwenda Shelisheli, huku mshambuliaji wa pembeni wa timu hiyo, Emmanuel Martins akiamini wenyeji wao St Louis watakufa mapema katika mechi yao ya marudiano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Martin alisema uwepo kwa Juma Mahadhi, Ibrahim Ajib, Geofrey Mwashiuya, yeye na Kabamba Tshishimbi pamoja na nyota wengine wa timu yao, hawaoni chochote cha kuwazuia kuwang’oa St Louis waliolala jijini Dar es Salaam kwa bao 1-0.

Mchezaji huyo alisema kile walichokionyesha Mwashiuya na Mahadhi aliyefunga bao pekee wakitokea benchi, kitaendelezwa kwenye mechi ya ugenini itakayopigwa Jumatano Uwanja wa Lenite mjini Victoria. “Wote tupo kwa ajili ya timu naamini umakini wao wa kuusoma mchezo ulitusaidia nyumbani na utatusaidia pia ugenini, hivyo hatuna hofu yoyote,” alisema.

Akiizungumzia michuano hiyo, Martin alisema inazidi kuwajengea uzoefu, huku akisisitiza kama watafuzu hatua ya awali ni wazi watapata uzoefu wa kutosha kwa mechi zijazo ambazo ni ngumu kufuzu hatua ya makundi. Yanga inahitaji ushindi ama sare ya aina yoyote ili kufuzu raundi ya kwanza.