Du! Nyota Majimaji wameigomea Yanga

Muktasari:

Kwa mujibu wa Kocha wa timu hiyo, Habibu Kondo mpaka jana asubuhi alikuwa amebaki na kikosi cha pili hivyo ikamlazimu kuongeza wachezaji wengine 14 kutoka timu yao ya vijana ili kuwawezesha kucheza na Yanga.

WACHEZAJI wa kikosi cha kwanza cha Majimaji- Songea, wamejiengua na kususa kucheza mechi ya Kombe la FA dhidi ya Yanga ikielewa ni shinikizo la madai yao ya fedha za usajili na mishahara.

Kwa mujibu wa Kocha wa timu hiyo, Habibu Kondo mpaka jana asubuhi alikuwa amebaki na kikosi cha pili hivyo ikamlazimu kuongeza wachezaji wengine 14 kutoka timu yao ya vijana ili kuwawezesha kucheza na Yanga.

Akizungumza kwa sauti ya kukata tamaa, Kondo alisema changamoto hiyo inamuumiza akili na ilianza muda mrefu wachezaji kugoma, wengine wakafukuzwa na walioondoka kabisa kwenye timu.

“Songombinde hii ilianza baada ya mechi na Njombe, wachezaji wakaondoka, na wengine wakafukuzwa, huku wengine wakigoma, tulishindwa kuanza mazoezi kabisa mpaka nilipochagua wale wa timu B, tumeanza kujiandaa leo (jana Ijumaa),” alisema yakiwa ni masaa machache kabla ya kukutana na Yanga hapo kesho.

Alisema anajua mechi itakuwa ngumu, kwani amejikuta na wakati mgumu wa kuunda kombinesheni ya haraka, lakini anaamini watapambana kadri wawezavyo kwenye mchezo huo.

Akizungumzia madai ya wachezaji hao Mwenyekiti wa Majimaji, Steven Ngonyani, alisema ni kweli wanadaiwa lakini wamepambana kwa nguvu zao kuhakikisha wanapata mishahara ili kuokoa jahazi huku pesa za usajili wanamsikilizia mbunge wao, Damas Ndumbaro.

“Kuhusu fedha za usajili Mbunge alisema atalitatua, ila kila kitu lazima kiende kwa utaratibu na mipango, ndio kwanza ameingia hivyo lazima aangalie anaanzia wapi ili aweze kulitatua jambo hili na ndivyo alivyotuambia.

Kwa upande wa mishahara tumepambana kupata mtu wa kuweka sawa jambo hilo,” alisema.