Djuma hataki majina Simba

KOCHA msaidizi wa Simba, Masoud Djuma amesema, hawezi kumchezesha mchezaji kwa sababu ya ukubwa wa jina lake na atakachokiangalia ni uwezo tu.

Djuma amezungumza hilo na kutolea mfano kwa wachezaji wake, Emmanuel Okwi raia wa Uganda na Mrundi Laudit Mavugo.

"Wakati wa maandalizi yetu Morogoro  nilimpa nafasi ya kucheza Okwi kutokana na kiwango kizuri alichokuwa anakionyesha mazoezini na nilipokaa na kuzungumza naye, alinihakikishia hata nikimpa nafasi ya kucheza atafanya vizuri na ndivyo alivyofanya katika mchezo wetu na Singida,"anasema Djuma ambaye katika mchezo huo walishinda mabao 4-0.

"Isingekuwa jambo rahisi kumpa nafasi ya kucheza huku kiwango chake kipo chini kwa sababu asingeweza kufanya alichokifanya. Mfano, sikumchezesha Mavugo katika mchezo ule ni kwa sababu nilimwona hakuwa vizuri, kila mtu anafahamu yule ni Mrundi mwenzangu na ingewezekana  ningempa nafasi hiyo kwa ajili ya undugu, lakini kamwe siwezi kufanya hivyo.

"Kama nafanya hivyo simsaidii, bali nakuwa namuumiza yeye anachotakiwa kufanya ni kujituma ili awe vizuri na afanye vizuri zaidi katika mechi atakazopata nafasi."