Dar yaibeba Tanzania bonanza la maveterani Afrika

Muktasari:

Mashindano hayo yanashirikisha timu za kutoka katika mataifa ya DR Congo, Rwanda, Uganda, Kenya na wenyeji Tanzania

Mwanza. Timu za Mkoa wa Mwanza, Mwanza Veteran na Rock City zimeshindwa kufurukuta kwenye bonanza la Maveterani kutoka Afrika Mashariki na Kati baada ya kupoteza michezo yake leo jioni kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.

Jumla ya timu nane kutoka mataifa ya DR Congo, Rwanda, Uganda, Kenya na wenyeji Tanzania zilikuwa zikishiriki bonanza hilo, ambapo kwa Tanzania timu ya Mpakani Dar es Salaam ndio imefuzu hatua ya nusu fainali.

Mwanza veteran imetolewa baada ya kupoteza michezo yake mitatu dhidi ya Vision 2020 ya Rwanda kwa mabao 6-1, kisha kupigwa mabao 4-1 dhidi ya Nile FC ya Uganda na kulala tena kwa mabao 7-0 dhidi ya Lespaves ya Kongo.

Rock city wao waliondoshwa na Mpakani kwa mabao 2-0, kisha kuchapwa Mulindi FC mabao 2-0 na kulizwa tena mabao 3-1 na Victoria.

Kwa matokeo hayo, Vision 2020, Lesepaves,Mulindi FC na Mpakani Dar es Salaam zimefuzu kucheza nusu fainali kesho Jumapili kusaka timu zitakazocheza fainali na kumpata bingwa.

Akizungumzia mashindano hayo,Mwenyekiti wa bonanza hilo, Afrika Mashariki, Hajj Yusuph alisema lengo ni kujenga mahusiano baina ya mataifa hayo.