DPP bado anapitia jalada la vigogo TFF

Dar es Salaam. Upande wa utetezi katika kesi inayowakabili aliyekuwa Shirikisho la Soka la Tanzania (TFF), Jamal Malinzi(57), Katibu Mkuu wa TFF, Mwesigwa Selestine(46) na Mhasibu wa TFF,  Nsiande Mwanga(27) umemlalamikia Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kwa kuchelewesha kesi hiyo.

Alikiwasilisha malalamiko hayo leo kwa Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri wa Mahakama ya Kisutu, Wakili wa utetezi Dominician Rwegoshora alidai DPP amekuwa akipitia jalada la kesi hiyo kwa muda mrefu.

Amedai kesi hiyo imechukua muda mrefu ambapo washtakiwa wapo rumande kwa takribani miezi 8 sasa tangu walipofikishwa kwa mara ya kwanza Juni 2017.

Kwa kipindi chote hicho upande wa mashtaka umeendelea kueleza mahakama upelelezi bado haujakamilika kwa madai kuwa DPP bado unaendelea kupitia jalada hilo.

"Sisi mawakili na wateja wetu hatuna malalamiko yoyote dhidi ya mahakama tunaelewa inafuata sheria na taratibu na mahakama haijapewa mamlaka ya kulazimisha upande wa Jamuhuri useme upelelezi umekamilika," alieleza Wakili Rwegoshora.

Hivyo aliomba iwepo kwenye kumbukumbu za mahakama kuwa wao wanalia na ofisi ya DPP.

Wakili Nehemiah Nkoko alidai kuwa hati ya mashtaka ipo wazi ambapo inaonesha risiti nakiasi cha fedha zinazodaiwa kuibiwa hivyo wanata kuambiwa ukweli ni kitu gani kinachokwamisha upelelezi katika kesi hiyo kukamilika.

Alidai kuwa wateja wao wapo ndani wanaumia na wanahitaji kujua hatma ya kesi yao kama kufungwa wafungwe na kama kuachiwa waachiwe.

Wakili Abraham Senguji wa upande wa utetezi alidai kwa namna hati ya mashtaka jinsi  ilivyo imejitosheleza na hivyo aliiomba mahakama iamuru upande wa mashtaka tarehe itakayopangwa wake na mashahidi kwa ajili ya kuisikiliza kesi hiyo.

Vinginevyo wapewe ahirisho fupi ili wawasilishe hoja kuhusiana na mwenendo wa upande wa mashtaka jinsi unavyoiendesha kesi hiyo na mahakama itoe uamuzi.

Baada ya kutolewa kwa hoja hizo, Swai alidai kuwa ombi la kuleta mashahidi ili kesi ianze kusikilizwa haliwezekani kwa mujibu wa sheria.

Alidai kuwa wamekuwa wakiiharifu mahakama katika kila hatua ya upelelezi hivyo aliiomba mahakama isitoe amri kwa maombi yoyote ya upande wa utetezi.

Alibainisha kuwa jalada la kesi hiyo bado lipo kwa DPP na kwamba hawana nia ya kuichelewesha kesi hiyo na akaomba wapewe siku 14 ili walifuatilia jalada la kesi hiyo.

Hakimu Mashauri baada ya kusikiliza hoja hizo atatoa uamuzi Machi 15, 2018 wa nini kitafuata kwa kesi hiyo.

Katika kesi hiyo, Malinzi na wenzake wanakabiliwa na mashtaka 28 ya uhujumu uchumi ikiwamo kughushi na utakatishaji wa fedha dola za marekani 375,418.

Katika kesi hiyo Malinzi wanakabiliwa na mashtaka 28 huku wenzake wakikabiliwa na makosa yasiyozidi manne.

Wakati kesi hiyo ikitajwa washtakiwa wote walikuwapo mahakamani na wanatetewa na Mawakili  Nehemia Nkoko, Dominician Rwegoshora na Abraham Senguji.