Coutinho halisi ndio huyu hapa

Muktasari:

Staa huyo wa Kibrazili ametua Nou Camp na kusaini mkataba wa miaka mitano na nusu baada ya Barcelona kulipa Euro 160 milioni kupata saini yake kutoka Liverpool.

BARCELONAHISPANIA. PHILIPPE Coutinho amefichua kwamba kwa sasa anaishi ndoto yake baada ya kusaini kujiunga na Barcelona inayoshiriki mikikimikiki ya La Liga.

Staa huyo wa Kibrazili ametua Nou Camp na kusaini mkataba wa miaka mitano na nusu baada ya Barcelona kulipa Euro 160 milioni kupata saini yake kutoka Liverpool. Ada hiyo ya uhamisho inamfanya Coutinho kuwa mchezaji wa tatu ghali duniani baada ya Neymar, aliyenaswa kwa Euro 222 milioni na Paris Saint-Germain akitokea Barcelona na Kylian Mbappe. Mkataba wa Coutinho umewekwa kipengele kinachohitaji kulipwa Euro 400 milioni kama kutakuwa na timu itakayohitaji kumsajili kutoka Barcelona kabla ya mkataba wake huo kufika mwisho.

Wakati mashabiki wa Barcelona wakimsubiri kumwona ndani ya uwanja staa wao huyo mpya akianza kuitumia timu yao, haya hapa mahojiano ya ana kwa ana yaliyofanywa na supastaa huyo wa Kibrazili. Barcelona inaongoza msimamo wa La Liga baada ya kuvuna pointi 51 katika mechi 19 ilizocheza, imeshinda mara 16 na kutoka sare mara tatu na hainapoteza mechi yoyote kwa msimu huu ikiwa chini ya kocha Ernesto Valverde.

Swali: Umefurahi?

Coutinho: Sana. Nimefurahi sana kuweza kuwa hapa

Swali: Ulishawahi kuwaza kwamba ukiwa na umri wa miaka 25 utakuwa kwenye jezi ya Barca? Je, hii ilikuwa zawadi nzuri ya Krismasi?

Coutinho: Ndiyo, siku zote hiyo ilikuwa ndoto yangu kubwa, tangu nilipokuwa mdogo sana kwa sababu ya historia ya klabu, kwa sababu klabu ni kubwa. Siku zote ilikuwa ndoto yangu kuvaa jezi ya Barca na hii leo nipo hapa, nimefurahi sana.

Swali: Uliishi Barcelona mwaka 2012 ulipokuwa ikiichezea Espanyol

Coutinho: Ndiyo

Swali: Unapenda kitu gani katika jiji la Barcelona?

Coutinho: Niliishi hapa kwa miezi 5 au 6. Jiji ni zuri. Nilipokuwa naishi hapa, nililipenda jiji kama nilivyokuwa nalipenda jiji la Rio, mahali ninakotokea. Ni jiji ninalolipenda kweli kweli.

Swali: Coutinho yupoje ndani na nje ya uwanja?

Coutinho: Ndani ya uwanja, siku zote nimekuwa nikijaribu kuonyesha ubora wangu katika kila mchezo na kila ninapopata nafasi. Najaribu kuonyesha ubora wangu kuisaidia timu kushinda. Najaribu kucheza kwa furaha. Nje ya uwanja, nipo kimya sasa. Nina binti, nimeoa na napenda maisha ya kuwa kimya.

Swali: Umeonekana umetulia, unasema kuhusu utambulisho wako. Unawasiwasi au umetulia tu?

Coutinho: Nimekuwa na wasiwasi sana siku chache zilizopita wakati wakuja Barcelona na bado nimekuwa na mshawasha wa aina hiyo hasa kwenye utambulisho wangu.

Swali: Unapenda kufanya nini katika muda wako wa ziada?

Coutinho: Napenda kuwa na familia yangu. Kucheka na kutabasamu ni kitu muhimu katika maisha yangu. Najaribu kuwa mwenye furaha nikiwa na watu wangu ninaowakubali.

Swali: Unapanda kusikiliza muziki wa aina gani?

Coutinho: Napenda kila kitu. Muziki wa Kibrazili kama vile pagode na samba. Napenda ala za reage ya Kihispaniola pia. Napenda muziki wa aina tofauti.

Swali: Kuna wimbo wowote unaoupenda?

Coutinho: Nitakutajia mstari mmoja tu kwenye huo wimbo ‘ni Mungu ndiye anayechagua staa na lazima atang’ara.’

Swali: Unapenda kula nini?

Coutinho: Napenda wali na maharage ya Kibrazili, lakini napenda kuonjaonja kila kitu.

Swali: Unaonekana unapenda sana tattoo?

Coutinho: Ninazo kadhaa. Nilianza kwa kuandika majina ya wazazi wangu, nikamwongeza mke wangu wakati tulipooana. Nina tattoo kubwa kabisa ya picha ya binti yangu, yenye maana kubwa sana kwangu. Pia nina tattoo moja yenye maneno “Usichoke kuota”. Naipenda sana.

Swali: Je, ulikuwa na shujaa yeyote wakati unakua?

Coutinho: Shujaa wangu siku zote alikuwa Ronaldinho. Brazil kuna wachezaji wengi sana mahiri; Romario, Ronaldo na Rivaldo, wachezaji ambao nilikuwa nikiwatazama wakicheza wakati nakua.

Swali: Unapenda mavazi gani; fasheni au kawaida tu?

Coutinho: Mimi nipo simpo. Napenda kuvaa simpo tu. Leo nimevaa suti ili kuonekana tofauti kidogo.

Swali: Unazungumza Kihispaniola?

Coutinho: Kidogo, ila naelewa kila kitu

Swali: Na umejifunza Kicatalunya?

Coutinho: Ni lugha ngumu, lakini nafahamu kusema ‘Visca el Barca’.

Swali: Unapenda wanyama?

Coutinho: Ndiyo, nina mbwa wawili nyumbani. Mmoja wa kutoka Barcelona.

Swali: Unapenda kutumia mitandao ya kijamii au kushea komenti za mashabiki?

Coutinho: Ndiyo, napenda kuposti picha za familia yangu, kile ninachofanya, nikiwa mazoezini, kwenye mechi. Napenda kushea mambo yangu mazuri.

Swali: Kuna sehemu yoyote unaipenda?

Coutinho: Sehemu ninayoipenda ni uwanjani

Swali: Bao lao utalidedicate kwa nani?

Coutinho: Kwa familia yangu, mke wangu na binti yangu ambao siku zote wamekuwa wakinisapoti ambao pia nimekuwa mwenye imani kubwa sana na siku zote namshukuru Mungu.

Swali: Je, kitu gani unakiwishi?

Coutinho: Kuichezea Barcelona na kuwa bingwa na kubeba mataji

Kila heri;

Coutinho: Nashukuru.