Cosafa yamwandaa kiungo Mbeya City

Dar es Salaam. Kiungo wa Mbeya City, Raphael Daudi amesema mashindano ya Cosafa yamemsaidia kumjenga kujiamini zaidi.

 Kiungo huyo anayetajwa kutakiwa na Yanga endapo atajiunga na mabingwa hao anategemea kupata ushindani mkali wa namba na kiungo mkongwe wa Thaban Kamusoko ndani ya kikosi cha Wanajangwani.

Alipoulizwa kama tayari ameishasaini Yanga, iliyokuwa ikimsubiria kutoka Afrika Kusini, alijibu "mpango huo upo, ila bado sijakamilisha, nikiwa tayari nitawajulisha."

Raphael aliliambia MCL Digital leo, Jumatatu kuwa kushiriki kwake mashindano ya Cosafa, kumepa ujasiri wa kujiamini kwamba anaweza kukabiliana na changamoto za kila aina atakazokutana nazo msimu ujao.

"Nimejifunza mengi katika Cosafa, kuanzia kwa wachezaji niliokuwa nao pamoja na timu zilizoshiriki jinsi ambavyo zilikuwa zinapambana kuonyesha vitu vya tofauti na kwamba soka lina heshima yake," alisema kiungo huyo.

Kitendo cha kocha wa Stars, Salum Mayanja kumpa nafasi ya kucheza ndani ya kikosi chake, alikiona kama kimefika wakati mwafaka kwake akitoa sababu ya msimu unaokuja anauona una jipya pia ushindani kuwa mkali. 

"Siwezi kufunguka zaidi, msimu ujao itajulikana kwa nini nasema nimepata ujasiri na kujiamini kupitia Cosafa, iliyoniongezea hatua nyingine."