JKT Mgambo, African Sport zapikwa kupanda Ligi Kuu

Muktasari:

Kocha wa timu ya Coastal Union Juma Mgunda  na mchezaji wa zamani wa timu ya Mtibwa ambaye kwa sasa ni Kocha wa Vibaoni United, Ezekiel Mhina  wamesema wanaweka mikakati ya kupandisha daraja timu hizo kwenda Ligi Kuu.

Handeni. Mikakati inazidi kuimarishwa ili kuziwezesha timu za JKT Mgambo ambayo ipo daraja la kwanza na African Sports iliyopo daraja la pili za jijini Tanga kupanda Ligi Kuu Tanzania Bara.
Kocha wa timu ya Coastal Union Juma Mgunda  na mchezaji wa zamani wa timu ya Mtibwa ambaye kwa sasa ni Kocha wa Vibaoni United, Ezekiel Mhina  wamesema wanaweka mikakati ya kupandisha daraja timu hizo kwenda Ligi Kuu.
Mgunda alisema kuwa Tanga vipaji vipo, hivyo baada ya Coastal kupanda daraja msimu huu, timu inayofuata ni African Sport na Mgambo JKT ili hadhi ya mkoa katika soka irudi kama zamani.
Alisema katika mkoa wa Tanga kuna vipaji vingi hasa mpira wa miguu hivyo ni vizuri kuimarisha timu zilizopo kupanda daraja ili kuleta hamasa kwenye timu ndogo ziweze kufanya vizuri.
 “Tunajipanga timu yetu ya Coastal Union isishuke  lakini pia kuziamshwa African Sports na JKT Mgambo nazo zipande daraja na kuleta heshima ya soka katika mkoa wa Tanga kama ilivyokuwa zamani,” alisema Mgunda.
Kocha wa Vibaoni United, Ezekiel Mhina alisema ikiwepo bajeti ya kutosha katika timu wachezaji ni lazima wafanye vizuri kwani watakuwa wanatimiziwa mahitaji yao ya msingi na kuweza kufanya mazoezi na kucheza bila misuguano yoyote.
Hivyo alishauri timu ziwekewe bajeti nzuri na kama kuna shida basi watafute wadhamini kufadhili timu katika msimu mzima kwa kufanya hivyo timu itaweza kufanya vizuri.
Mchezaji wa Umoja FC, Saidi Mhina alisema pia ni vizuri TFF kuwafuatilia  baadhi ya marefa kwani wapo wenye tabia ya kukubali kununuliwa na kuuza mechi badala ya kuangalia vipaji.
Katika msimu wa Ligi Kuu uliopita timu ya Coastal Union, African Sport na JKT Mgambo za mkoa wa Tanga, zote zilishuka daraja na katika msimu huu Coastal Union imepanda.