Chirwa njia nyeupe Simba

Muktasari:

Hata hivyo imebainika Simba imepania kumvutia straika huyo Msimbazi na tayari mazungumzo baina ya pande mbili yamekuwa yakifanyika kwa usiri mkubwa, japo Mzambia ameweka misimamo mikali juu ya usajili huo mpya kwake.

KAMA unadhani Simba inatania kuhusu ishu ya Mzambia Obrey Chirwa wa Yanga soma hapa. Kwa wiki kadhaa sasa, Chirwa amekuwa akihusishwa na Simba huku mwenyewe akisisitiza kwamba hakuna mpango kama huo wa msimu ujao kuvaa uzi wa rangi nyekundu na nyeupe.

Hata hivyo imebainika Simba imepania kumvutia straika huyo Msimbazi na tayari mazungumzo baina ya pande mbili yamekuwa yakifanyika kwa usiri mkubwa, japo Mzambia ameweka misimamo mikali juu ya usajili huo mpya kwake.

Inaelezwa, Chirwa amekuwa akiwasisitiza mabosi wa Simba wanaotaka kumlainisha mapema kutua Msimbazi baada ya mkataba wake na Yanga kumalizika mwishoni mwa msimu huu, kuwa wamuache kwanza kwani anafikiria kucheza nje ya Tanzania.

Hata hivyo, mabosi wa Msimbazi ni kama hawamwelewi kwa vile kwa sasa mipango yao ni kuhakikisha wanakuwa na straika huyo kutokana na kuonekana anawafaa zaidi kwa soka inalocheza chini ya makocha Pierre Lechantre na Masudi Djuma.

Simba inamtamani Chirwa kwa sababu mastraika wake wawili; Laudit Mavugo na Juma Liuzio wanashindwa kufanya vema na kuacha kazi ya kutupia nyavuni kufanywa na akina Emmanuel Okwi na John Bocco, jambo lisilovutia kwa afya ya timu.

Benchi la Ufundi la Simba kupitia Kocha Msaidizi, Djuma, limefichua sifa tano za Chirwa zinazosabisha kuwashawishi vinara hao wa Ligi Kuu Bara kutaka kumnasa Mzambia huyo katika usajili wa msimu ujao.

Kocha Djuma alitaja mambo hayo matamu muhimu aliyonayo Chirwa na kuonekana anaweza kuisaidia Simba kuwa ni, uwezo wa kusaidia wachezaji wenzake kufunga uwanjani kutokana na kipaji kikubwa cha kujipanga na kuwasoma mabeki.

Sababu ya pili alisema Chirwa ana uwezo wa kuwasumbua mabeki hata akiwa pekee yake kitu ambacho uwepo wake uwanjani ni faida kubwa kwa timu, lakini pia uwezo wa kumiliki mpira hata akiwa amezongwa na watu wengi ni jambo jingine.

“Pia ni mfungaji mzuri wa mabao, anatoa pasi kwa wenzake na pia anajua kuitafutia timu ushindi. Anajua kutumia nafasi na hata timu yake ikicheza mechi ngumu anabaki na mpira na kuwasumbua wachezaji wengi wa upinzani.

“Binafsi namuona Chirwa kama mshambuliaji wa aina ya kipekee mambo yote ambayo straika anatakiwa kuwa nayo yeye anayo, kiukweli ni miongoni mwa

mastraika bora hapa nchini,” alisisitiza kocha huyo raia wa Burundi.

JUUKO, GYAN

Simba ipo katika mbio za ubingwa wa Ligi Kuu Bara na moja ya lengo lao kuu msimu huu ni kutwaa ubingwa ili mwakani wapate nafasi ya kushiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika ambayo zaidi ya mara tatu watani zao wa Yanga wamekuwa wakishiriki.

Mmoja wa viongozi wa Simba aliyeomba kuhifadhiwa jina alifichua kuwa iwapo watabeba ubingwa wa Ligi Kuu watafanya mchujo kwa nyota wao wa kigeni hasa waliochemsha msimu huu akiwemo Mavugo, Juuko Murshid na Nicholas Gyan.

“Wenye uhakika wa kubaki kikosi mpaka sasa kwa nyota wa kigeni ni Okwi, Asante Kwasi, James Kotei na Haruna Niyonzima ambaye japo hajacheza kutokana na kuwa majeruhi bado tunaamini uwezo wake ni mkubwa hata akipona ataisaidia timu,” alisema bosi huyo.

“Ila hao wengine uwezekano wa kuwa nao ni mdogo mno, sijui labda kama watakuwa na mabadiliko.”