Chelsea yaifukuzia Man City mbio za ubingwa

Muktasari:

Matokeo hayo ni faraja kwa kocha Mtaliano Antonio Conte ambaye wiki hii amepamba vyombo vya habari.

London,England.Eden Hazard ameongoza mauaji ya Chelsea dhidi ya Burnley katika mchezo wa Ligi Kuu England jana Jumapili.

Chelsea ikiwa ugenini, ilipata mabao 4-0 katika mchezo ambao nahodha huyo wa Ubelgiji, alifunga mawili.

Mabao mengine yalifungwa na Willian na Victor Moses aliyefunga dakika moja kabla ya mpira kumalizika.

Matokeo hayo ni faraja kwa kocha Mtaliano Antonio Conte ambaye wiki hii amepamba vyombo vya habari.

Conte ameibua mjadala baada ya kudai anataka kumsajili mshambuliaji mrefu Peter Crouch wa Stoke City.

Muda mfupi baada ya kutoa taarifa ya kumtaka mchezaji huyo wa zamani wa Liverpool, mashabiki wa Chelsea walimjia juu kocha huyo wakidai hana jipya.

Mbali na Crouch, kocha huyo wa zamani wa ‘Kibibi Kizee’ cha Turin Juventus alimtupia ndoano Andy Carroll wa West Ham United.

Hata hivyo, kocha wa West Ham United, David Moyes alimuonya Conte akimtaka asicheze kamari kumsajili Carroll kwa kuwa anatarajiwa kufanyiwa upasuaji.

Lakini, jana aliwajibu mashabiki kwa kuwapa ushindi mnono ambao umeipa Chelsea pointi muhimu katika mchuano wa kuwania ubingwa msimu huu.