Cheki Salah alivyogeuka shujaa halisi wa soka la Misri

Tuesday February 13 2018

 

CAIRO, MISRI. WINGA wa Liverpool, Mohamed Salah ameliteka soka la England katika mwendo wa kushangaza.

Haikutazamiwa kama angeonyesha makali haya wakati aliponunuliwa na Liverpool kutoka Roma kwa dau la Pauni 37 milioni katika dirisha kubwa lililopita la majira ya joto.

Wakati Salah akionekana kuwa shujaa machoni mwa mashabiki wa Liverpool, lakini nyumbani kwao Misri Salah ni zaidi ya shujaa wa kawaida na amekuwa akiwapagawisha raia wa nchi hiyo ambao wanamuona ana mchango mkubwa kwao katika maisha ya kawaida.

Ushujaa wa Salah tayari ulikuwa wazi kwa raia wa Misri kabla hata hajafunga mabao mawili, ikiwemo moja la penalti katika pambano la kufuzu Kombe la Dunia 2018 litakayofanyika Russia dhidi ya DR Congo jijini Alexandria Oktoba mwaka jana.

Kwa mabao hayo ya Salah, Misri ilifanikiwa kutinga katika fainali za Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza tangu ilipofanya hivyo mara ya mwisho mwaka 1990 ambapo ilikwenda Italia.

Pamoja na uhodari wake mkubwa uwanjani, Salah ambaye anaishi maisha ya kawaida hajasahu jinsi ambavyo mizizi ya alikotokea ambayo imemfanya leo awe shujaa wa Taifa la Misri. Shule yake aliyosoma utotoni katika Mji wa Basyoun pamoja na baadhi ya mitaa imepewa jina lake kwa heshima yake.

Ameendelea pia kuwa na uhusiano mzuri na Mji wa Nagrig uliopo Gharbia Kaskazini mwa nchi ya Misri.

Mara kadhaa amekuwa akitumia pesa yake ya mfukoni kwa ajili ya kuwalipia shule pamoja na gym mastaa wajao wanaotoka katika mji huo.

Januari mwaka huu, Salah alipokewa na Rais wa Misri, Abdel Fattah Al-Sisi pamoja na Waziri wa Vijana na Michezo wa Misri, Khaled Abdel Aziz akipongezwa kwa mafanikio yake pamoja na mchango wake wa Pauni za Misri 5 milioni ambazo ni sawa na Pauni 200,000 alizotoa katika mfumo wa kuimatrisha maendeleo wa Taifa la Misri unaojulikana kama Tahiya Misri (Tahiya Masr).

Salah pia alichangia kiasi cha Euro 30,000 katika chama cha wachezaji wa zamani wa Misri na alipopewa zawadi ya jumba la kifahari na Mfanyabiashara mmoja mkubwa nchini humo kama zawadi yake kwa mabao aliyofunga dhidi ya Congo na kufuzu Kombe la Dunia, alikataa zawadi hiyo na badala yake akaomba pesa kwa ajili ya kuchangia maendeleo ya mji wake aliotoka.

Salah amekuwa akitumika kama kiunganishi cha watu wa Misri na soka lao kwa sababu kabla hajaenda Ulaya alikuwa akichezea Klabu ya Arab Contractors (El Mokawloon). Hakuchezea klabu mbili kubwa nchini humo, Al Ahly na Zamalek, na hilo linamfanya apendwe na watu wa pande zote katika soka la Misri.

Alipokuwa na umri wa miaka 14, Salah alikuwa anasafiri kwa basi zaidi ya saa nne kwa ajili ya kwenda kufanya mazoezi na klabu yake ya Arab Contractors. Alikuwa anatumia saa hizo kwenda na kurudi nyumbani kwao. Leo, Salah amekuwa staa mkubwa kwao lakini bado anaishi maisha ya kawaida tu.

“Ni mtu mpole sana, mwanasoka mkimya na mtu muungwana. Mara chache kumkuta anazungumza na vyombo vya habari vya Misri au nje ya nchi,” anasema mwandishi mkongwe wa soka la Misri, Marween Saeed.

“Anatumia mitandao ya jamii mara chache. Hapendi kuongea sana na hilo ni jambo jema kwa sababu mara nyingi tunaona mastaa wanaongea mambo ambayo hawakupaswa kuyaongea katika TV au kutuma mitandaoni,” anaongeza mwandishi huyo.

“Mo alioa akiwa katika umri mdogo na amebarikiwa kuwa na mtoto wa kike na mara zote amemuondoa katika macho ya watu. Kuna mitaa na taasisi ambazo zimepewa majina yake baada ya ushujaa wake usiotazamiwa wa kutupeleka katika Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza tangu mwaka 1990. Misri imebarikiwa kuwa na kipaji kama cha Salah na yeye amekuwa zawadi ambayo inajitolea.”

Hisia kwamba Salah hatavimba kichwa kutokana na sifa anazopewa sasa zinarudiwa na mtu ambaye alimfundisha kwa mara ya kwanza baada ya kuondoka Misri na kutua Ulaya mwaka 2012 kutimiza ndoto zake.

Mtu huyo ni Murat Yakin, kocha wa zamani wa klabu yake ya Basel ya Uswisi ambaye kwa sasa ni kocha wa Grasshopper ya hapo hapo Uswisi. Kocha huyo alikuwa Basel wakati Salah alipofunga mabao ya ushindi dhidi ya Chelsea ya Jose Mourinho katika mechi za makundi Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu wa 2013-14.

Kutokana na mabao hayo, Chelsea ilimnunua Salah kwa dau la Pauni 11 milioni Januari 2014 ingawa tayari Liverpool ilishakubaliana na Basel kumchukua staa huyo.

“Mo ni mpole na muungwana sana. Ni mtu mkimya lakini pia amekuwa na huruma nje ya uwanja. Lakini ndani ya uwanja ni kiongozi, ana kipaji na mpambanaji,” anasema Yakin.

Yakin, ambaye alikuwa kocha wa Basel kati ya Oktoba 2012 na Mei 2014, alitabiri mapema kuondoka kwa Salah na kwenda juu zaidi wakati alipofunga bao dhidi ya Tottenham katika robo fainali ya Kombe la Europa dhidi ya Tottenham.

“Kama Mohamed anaweza kufunga, basi anaweza asicheze tena hapa. Kwa muda huu, Mo ni mchezaji safi sana na atajifunza na kufanyia kazi soka lake. Akiendelea hivi hivi atakuwa hatari zaidi na zaidi,” alisema Yakin.

Salah amekuwa mchezaji wa kwanza kufunga mabao 20 ya Ligi Kuu ya England kwa Liverpool ndani ya mechi chache. Mabao yake mengi ya kusisimua ukianzia kwa shuti la mbali alilomtungua kipa wa Manchester City, Ederson baada ya kuhamisha mpira ovyo. Lakini pia bao lake la pili katika pambano dhidi ya Spurs liliwaacha mashabiki midomo wazi.

Kipaji chake kimefuta maswali ya mashabiki na wachezaji wa zamani wa Liverpool ambao walikuwa wanahoji umakini wa timu yao kumchukua mchezaji ambaye anaonekana kama vile alichemsha katika Ligi Kuu ya England wakati akiwa na Chelsea.

Staa wa zamani wa Liverpool na Timu ya Taifa ya Sweden, Jan Molby anakiri Salah amemshangaza kwa kiasi kikubwa kutokana na kipaji chake ambacho anaonyesha.

“Amenishangaza na siangalii sana kwa alichofanya au ambacho hakufanya Chelsea. Zaidi naangalia nilichokiona akiwa na Roma,” anasema Molby.

Vyovyote itakavyokuwa Salah amekuwa na msimu mzuri zaidi Liverpool bila ya matarajio ya wengi. Kwa sasa wengi wanamuangalia yeye na mastaa wenzake wa Misri jinsi watakavyofanya mambo katika fainali za Kombe la Dunia, Russia Juni mwaka huu.