Chama la Wana yaapa kuvunja mwiko

Muktasari:

  • Chama la Wana lenye maskani yake mjini Shinyanga imecheza mechi nane Uwanja wa Sokoine, lakini hawajawahi kushinda.

STAND United ‘Chama la Wana’, haijawahi kupata ushindi Uwanja wa Sokoine, Mbeya tangu ipande Ligi Kuu lakini imetamka wazi sasa imetosha na leo Jumapili lazima waicharaze Mbeya City katika mchezo utakaopigwa jijini humo.

Chama la Wana lenye maskani yake mjini Shinyanga imecheza mechi nane Uwanja wa Sokoine, lakini hawajawahi kushinda.

Uwanja huo unatumiwa na timu za Prisons na Mbeya City na timu hiyo licha ya kujitutumua mbele ya wenyeji wao jijini humo uishia kutoka kapa.

Kocha Msaidizi wa Stand, Augustino Malindi alisema leo Jumapili ndio itakuwa mwisho wa wao kuondoka Mbeya bila kupata pointi tatu.

Alisema wanajua fika mchezo wao na Mbeya City utakuwa mgumu, lakini tayari wamejipanga kuhakikisha wanaondoka na ushindi kama walivyofanya mbele ya Singida United kwenye Uwanja wa Namfua, Singida wikiendi iliyopita.

“Hatujawahi kupata pointi tatu Mbeya tangu tumepanda Ligi Kuu, ila tumejipanga safari hii lazima tuondoe mkosi kwa kupata ushindi wa kwanza Sokoine,” alisema.

Kocha Malindi alisema kipa wao Frank Muwonge aliyeugua ghafla wakati wa mchezo wao na Singida United, amerejea upya uwanjani.