Cavani, Neymar wafanya kufuru PSG

Paris, Ufaransa. Mshambuliaji Edinson Cavani ameifikia rekodi ya Zlatan Ibrahimovic huku Neymar akifunga mabao manne wakati Paris Saint-Germain ikichakaza Dijon kwa mabao 8-0.

Mshambuliaji Cavani alifunga bao lake la 156, akiwa na klabu hiyo, lakini Neymar aliuteka mchezo huo kwa kufunga mabao manne peke yake.

Angel Di Maria alifunga mabao mawili, huku Kylian Mbappe akifunga moja katika kalamu hiyo inayowafanya PSG kuongoza ligi kwa tofauti ya pointi 11 kwa Lyon inayoshika nafasi ya pili.

Di Maria alitumia vizuri pasi ndogo ya juu ya Neymar kufunga bao la kwanza katika dakika ya nne, kabla ya kuongeza bao la pili.

Di Maria alitengeneza krosi nzuri iliyomkuta Cavani na kufunga bao lililomfanya kuwa sawa na Ibrahimovic.

Neymar aliongeza bao nne kwa mpira wa adhabu uliokwenda moja kwa moja wavuni katika mechi hiyo iliyokuwa ya upande moja.

Baada ya Di Maria kupoteza nafasi ya kufunga bao la tatu wakati Mbappe alipoingia, Neymar alifunga bao lake lingine la juhudi binafsi.

Pia, Mbrazil huyo alitegeneza pasi ya bao la Mbappe alilofunga ikiwa ni pasi ya bao ya 11, kutolewa na Neymar akiwa ni mchezaji pekee aliyetegeneza pasi nyingi za mabao katika Ligi Kuu tano kubwa Ulaya.

Cavani aliangushwa katika eneo la penalty, pamoja na mashabiki kutaka mshambuliaji huyo aipige ili ivunje rekodi ya Zlatan, lakini Neymar alichukua jukumu hilo na kufunga bao la nne.