Bushiri aanza kuchonga Njombe Mji

Dar es Salaam. Kocha wa Njombe Mji, Ally Bushiri amesema vijana wake wameanza kuelewa falsafa yake ya kucheza soka la kushambulia.

Bushiri aliyechukua mikoba ya Mlange Kabange aliyekuwa anakaimu nafasi ya Hassan Banyai, hajapoteza mchezo hata mmoja hadi sasa tangu alipochukua jukumu hilo.

“Kati ya vitu nilivyoanza kwa kuvifanyia kazi ni namna ya uchezaji, nilikikuta kikosi kikiwa hakina kasi kwenye ushambuliaji, nimekuwa muumini wa soka la kushambulia kwa kasi kipindi kirefu.

“Ushambuliaji wa kasi unamfanya mpinzani kufanya makosa bila ya kutegemea,” alisema kocha huyo wa zamani wa Mwadui ya Shinyanga.

Tangu Bushiri apewe majukumu ya kukinoa kikosi cha Njombe Mji, amewaongoza kwenye michezo mitatu ya Ligi Kuu Bara ambapo wametoka sare mara mbili dhidi ya Mbeya City 0-0 na Majimaji ya bao 1-1 na kushinda dhidi ya Ruvu Shooting kwa mabao 2-1.

Mbali na kuwaongoza kwenye michezo hiyo mitatu ya ligi pia kwa mara ya kwanza, Bushiri ameifanya Njombe Mji kuweka rekodi ya kutinga kwenye hatua ya robo fainali ya Kombe la FA kwa mara yao ya kwanza.