Wolper ndio basi tena

Tuesday May 9 2017

 

By RHOBI CHACHA

HUWEZI kuamini, lakini ndivyo ukweli ulivyo kuwa, lile penzi lililoibuka na kubamba kinomanoma na hasa kwenye mitandao ya kijamii kati ya mwigizaji nyota wa filamu nchini, Jacqueline Wolper na Harmonize limefikia tamati.

Achana na taarifa za awali ambazo baadaye zilikuja kubainika kuwa ilikuwa ni kiki ya kuipandisha chati kazi mpya ya mwimbaji huyo wa muziki wa kizazi kipya, safari hii ni Wolper ndio basi tena atafute chaka jingine la kupata malavidavi.

Harmonize amefichua ukweli juu ya kutemana rasmi na Wolper, japo mwanadada huyo wiki moja na ushei aliwahi kunukuliwa na Mwanaspoti kuwa, hakuna kitu kitakachomtenganisha na nyota huyo kutoka Wasafi Classic (WCB).

Hata hivyo, Harmonize amefichua kila kitu juu ya kutemana na Wolper, akisisitiza kuwa, safari hii sio kiki wala kitu gani, ila wametemana na mwenza wake huyo na kutamatisha mipango yote waliyokuwa wameitangaza wakati penzi lao lilipokuwa motomoto.

MSIKIE MWENYEWE

Harmonize amefichua uhusiano wao mwanzo mwisho kwa kufunguka hivi:

“Jamani ngoja niweke wazi hili suala na naomba watu waelewe leo na liishie hapa, tuendelee na masuala mengine, kwani kuongelea kitu kimoja kila siku inakuwa haipendezi kwani kuna vitu vingi vya kuongea.

“Wolper nimeshaachana naye na mapenzi yetu hayakuwa kiki wala maigizo kama baadhi ya watu wasiojua ukweli. Kwa kweli Wolper alikuwa mpenzi wangu na nilikuwa na malengo mengi naye, ila ndio hivyo malengo yamevurugika na kila mtu yuko kivyake kwa sasa,” anasema Harmonize.

Aidha Harmornize ameongeza kuwa, kuachana kwao sio sababu ya kushindwa kusalimiana au kuzungumza kwani, kuachana ni jambo la kibinadamu, hivyo hawajaweka uadui wowote baina yao, hivyo hata watu wakiwaona wako karibu wasifikiri ni wapenzi, bali wachukulie kama ni mtu na kaka yake au dada yake tu.

WOLPER KAMTOA

USHAMBA

“Unajua sipendi kuachana na mwanamke kwa visasi na hata nikiachana naye kwa staili hiyo wakitokeo lakini sio Wolper. Namaanisha kuwa Wolper ni mwanamke maalumu kwangu, kwani ndiye aliyenitoa ushamba. Nikisema hivyo nina maana kuna vitu vingi nilikuwa sivijui, nimevijua kupitia kwake, si unajua miye nimetokea kijijini, hivyo vitu vingi vya mjini sikuwa navifahamu, ndio maana nasema Wolper nitaendelea kumpa heshima yake katika maisha yangu na sitamdharau hata siku moja.”

CHANZO NINI?

Harmonize ameshindwa kabisa kuweka bayana kilichowafanya wafarakane na baby wake, ilihali walikuwa kama kumbikumbi tangu penzi lao lichipukie katikati ya mwaka jana.

“Naomba ieleweke tu nimeachana na Wolper, ila chanzo siwezi kusema kwani nitaonekana wa ajabu kuzungumzia ishu kama hii hadharani, sababu ya heshima niliyonayo kwake, siwezi kusema nimemkosea au amenikosea ila ifahamike tumeachana kwa amani na kupeana baraka zote, kila ashike lake.”

HAJAMTAMBULISHA UKWENI

Mwaka jana kuna habari zilizagaa kuwa Harmornize, alimpeleka Wolper kwao mjini Mtwara kwa ajili ya kumtambulisha kwa wazazi wake, lakini mwimbaji huyo amefichua kuwa hakuna kitu kama hicho, ili ilivumishwa tu na wanahabari.

“Sikuwahi kumtambulisha nyumbani kwetu, ila mama yangu alikuwa anajua tu, kuwa Wolper ni mpenzi wangu, hivyo wanaosema kuwa nilienda kumtambulisha Wolper labda ni kwa vile nilienda kufanya shoo nikiwa naye Mtwara,” anasema.

KUJUTIA MAPENZI

Harmonize kama binadamu wengine wenye moyo, anakiri kuwa aliwahi kuumizwa na kuyajutia mapenzi.

“Nimeshawahi kujuta sana na hapa naona kama unanitonyesha kidonda dah! Ila tuyaache tu, maana unaweza kumwamini mwanamke katika mapenzi na baadaye akaja kukutoa katika mudi ya mapenzi kwa kweli ni lazima ujute.”

KING’ASTI MPYA

Baada ya kutema na Wolper, mwimbaji huyo tayari ana king’asti mpya wa kutuliza mtima wake?

“Ndio nina mpenzi ila siwezi kumuweka wazi kwasasa kwasababu nimeshajifunza kutokana na makosa, huo ni utaratibu niliyojiwekea, sitaweza kuweka wazi uhusiano wangu kwa sasa hadi nitakaporidhia na kuamia kufunga ndoa.”

AJIWEKWA KWA

MZUNGU NINI?

Zipo habari mtaani na mitandaoni zimezagaa zikidai kuwa, kwa sasa Harmornize ana uhusiano na mwanamke wa Kizungu, aliyempa ujauzito na akiwa amemnunulia nyumba na gari, mwenyewe anasemaje?

“Kwanza ngoja nilizungumzie hili suala la nyumba, hivi siwezi kununua nyumba au gari? Hili naona linazungumziwa sana, yaani kwa shoo zote ninazofanya na kutoa kazi zinazobamba kwa mashabiki kweli nishindwe kumiliki nyumba au kununua gari? Basi nishindwe gari, yaani hata Bajaji nayo nishindwe, hapana! Jamanii watu waache hizo bwana!

“Kuhusu suala la kuwa na mwanamke wa Kizungu na kumpa ujauzito sio kweli, watu wanaongea tu kutaka kumjaza Wolper hasira na ilimradi waongee kwa vile yeye ana wafuasi (followers) wengi katika mitandao, ila sijampa mtu ujauzito tena natamani sana mtoto maana karibia wenzangu wote wa WCB wana watoto. Nami natamani niwe baba na Inshallah nitapata muda ukifika,” anasema.

UMRI KWAKE SIO ISHU

Harmonize amefichua katika mapenzi kwake huwa haangalii umri kwa sasa sio ishu kwake.

“Siangalii umri katika mapenzi, hivyo mwanamke yeyote mwenye sifa ninazohitaji ikiwamo upendo, kujali na uelewa sambamba na mvuto machoni kwangu, itakuwa freshi tu. Sitaangalia umri kwani mapenzi sio umri na ndio maana unaona kwa Wolper watu walisema sana, lakini sikuwasikiliza sababu ya sharti nililojiwekea, kwamba umri ni namba tu muhimu mapenzi shatashata,” anasema.