Usiku wa Mbalamwezi ulivyonoga

KATIKA vitu ambavyo hunoga sana Unguja na Pemba ni tamasha Usiku wa Mbalamwezi ‘Full Moon Party’. Ni burudani ambayo huwa na utamu wa aina yake kama ilivyo kwa Fiesta Tanzania Bara.

Wasanii na mastaa mbalimbali hukusanyika Zanzibar kulishuhudia kila tamasha hili ambalo hufanyika kwa mwezi mara moja huku wageni wa nje wakimiminika kwelikweli.

Ni tamasha ambalo limefanikiwa kuwaunganisha wanamuziki kutoka nchi mbalimbali duniani na kuitangaza Zanzibar kimataifa pamoja na kuinua utalii wa ndani kwa wageni wanaotoka Tanzania Bara na nchi jirani za Jumuiya ya Afrika Mashariki. Kivutio kikubwa kwenye tamasha hilo ni miziki ya asili ya Zanzibar na Kiafrika ambayo imekuwa ikiwavuta wengi kwa vile imekuwa adimu kwenye miaka ya karibuni haswa kutokana na ukweli kwamba, nyimbo nyingi ambazo zimekuwa zikipigwa kwenye jamii ni zile za kisasa zaidi.

Shoo hiyo hufanyika usiku kwenye ufukwe wa hoteli ya Kendwa Rocks, iliyopo ukanda wa mashariki wa Mkoa wa Kaskazini Unguja na kutoa burudani ya muziki pamoja na ngoma za asili na utamaduni zikipigwa na wasanii wakongwe wa visiwani hapa.

Inawezekana lisiwe maarufu zaidi Tanzania Bara, lakini kwa Unguja ni tamasha kubwa na Jumamosi ya Oktoba 15, mwaka huu, Tamasha la Mbalamwezi lilitimiza miaka 20  huku burudani zikiongozwa na bendi la Njenje na hivi sasa limekuwa mojawapo ya matamasha maarufu duniani likishika nafasi ya pili kwa ubora kati ya matamasha saba ambayo yamekuwa yakifanyika katika nchi mbalimbali.

Mwanzilishi wa tamasha hilo Ali Kilupi alisema lengo hilo ilikuwa ni  kutangaza  muziki na utamaduni wa Zanzibar kimataifa na kuwakusanya wasanii wenye vipaji tofauti.

Kilupi alisema tamasha hilo linafanyika wakati mwezi unapokuwa mkubwa (Full Moon), na linaweza kuleta tija zaidi kama litaangaliwa na kuenziwa kama alama ya kuitangaza Zanzibar kupitia utamaduni, muziki na sanaa.

“Lina miaka 20 sasa, tumepanda milima na kuvuka mabonde na hatimaye leo (juzi Jumamosi usiku) tumeweza kupata mafanikio makubwa na matokeo yake Full Moon Party imeitangaza Zanzibar na Tanzania kimataifa, na pia ni sherehe ya pili kwa ukubwa inayofanyika fukwe za bahari katika viwango vya ubora wa kimataifa,” alisema Kilupi.

Mbali na wasanii, viongozi wa serikali wamelazimika kuwa karibu na tamasha hilo na kushuhudia Usiku wa Mbalamwezi ukiwa umepambwa na burudani za aina mbalimbali akiwemo Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo, Chum Kombo Khamis, Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi, wadau wa sekta ya utalii pamoja na Mwenyekiti mstaafu wa Jumuiya ya Wawekezaji katika sekta ya utalii Abdulsamad Said Ahmed.

Usiku huo huadhimisha miaka 20 juzi ulipambwana na  burudani na matukio ya upigaji wa fashi fashi (Fire Works), katika ufukwe wa Kendwa huku midundo ya muziki ikipigwa kutoka usawa wa bahari na kufanikiwa kuwaunganisha wageni wa mataifa mbalimbali ambao, hushiriki tamasha hilo na kutoa mchango mkubwa wa uchumi.

Waziri wa zamani wa Wizara ya Nchi, Ofisi ya Waziri Kiongozi ambaye ni Mwakilishi wa Jimbo la Shauri Moyo Hamza Hassan Juma alisema; “Ajira zilizotokana na tamasha hilo ni kielelezo tosha kuwa lina faida na umuhimu mkubwa kwa wananchi wa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla, lakini linahitaji kutangazwa zaidi ili kuwavutia wageni wengine pamoja na wanamuziki wenye majina makubwa.”

Hata hivyo, alisema Serikali za Mkoa zina wajibu mkubwa wa kuwalinda na kuwaendeleza wawekezaji wazalendo, badala ya kuwawekea vikwazo katika uendelezaji wa muziki, hasa kwa kuzingatia kuwa linafanyika mara moja kwa mwezi na hakuna sababu za kuwekewa vikwazo kwa kulinda masilahi ya wawekezaji wageni.

Hata hivyo, Abdulsamad Said Ahmed ambaye ni mmiliki wa hoteli ya Sunset Beach Zanzibar alisema tamasha hilo limejizolea umaarufu mkubwa duniani kama yalivyo matamasha mengine ya Sauti za Busara na Tamasha la Nchi za Jahazi.

“Hoteli zote zimejaa wageni, hawa wote wamekuja kushuhudia Full Moon Party, ni tamasha ambalo linapaswa kuangaliwa kwa jicho la karibu, lina manufaa makubwa kwa wananchi na serikali, tunapokea wageni katika kipindi ambacho sio cha utalii (low season) kwa sababu ya tamasha hili Zanzibar imejitangaza kimataifa,” alisema Abdulsamad.

Wanamuziki waliotumbuiza katika tamasha hilo ni kutoka nchini Uingereza, Italia, Afrika Kusini, Tanzania Bara na Zanzibar ambao walionesha vipaji na wameacha hadithi kubwa kabla ya tamasha jingine kufanyika tena visiwani hapa.

Zaidi ya watu 1,000 wanakutanishwa na tamasha la Full Moon Party ambapo watu 250 wamenufaika na ajira mbalimbali.

Wasanii mbalimbali wa Bongo Fleva na Bongo Movie pamoja na wabunifu wa mitindo pia ni miongoni mwa watu wanaohudhuria tamasha hilo ambalo husababisha huduma za usafiri wa bahari na anga kuwa mgumu kutokana na wageni wengi wanaofika Zanzibar kushuhudia Usiku wa Mbalamwezi.