Q Chilla hawezi kusahau haya!

Q-CHILLA

Muktasari:

  • Ni wachache ambao hukataa ukweli katika mlolongo mzima wa maisha aliyopitia, pengine kwa kutaka kujisahulisha ama kujisikia vibaya.

MAISHA ni kama kitabu cha historia kwa kila binadamu kwani, hupitia milima na mabonde mpaka anapomaliza muda wake wa kuishi hapa duniani.

Kuna maisha ya furaha, huzuni na mengine ya kustaajabisha ambayo wakati mwingine mhusika hapendi hata kuyasikia kwa namna matukio aliyokumbana nayo yanapompa kumbukumbu isiyoweza kufutika kichwani mwake.

Ni wachache ambao hukataa ukweli katika mlolongo mzima wa maisha aliyopitia, pengine kwa kutaka kujisahulisha ama kujisikia vibaya.

Lakini, kuna wengine kama mwimbaji nyota wa muziki wa kizazi kipya nchini, Abubakar Katwila maarufu Q- Chilla ama Q Chief.

Mwanamuziki huyo mwenye sauti ya kumtoa nyoka pangoni na miongoni mwa waimbaji wazoefu nchini, anasema hawezi kusahau baadhi ya mambo yaliyowahi kumtokea nyuma ambayo kila akiyakumbuka hupatwa simanzi.

MAMBO YAPI?

Q Chilla anasema mambo asiyoyasahau na kila akikumbuka hujikuta akimwaga chozi, la kwanza ni pale akiwa na miaka 10 alipompoteza mama yake mkubwa akiwa ughaibuni nchini Botswana.

Anasema kila akikumbuka jinsi alivyoweza kusafiri na mwili wa mama yake huyo aliyemlea kwa mapenzi makubwa, huwa anajikuta akilia kwa sababu ilimuacha katika mateso makubwa kabla ya kuja kutulia na kufanya yake.

Anasema akiwa na miaka hiyo 10 alifiwa na mama yake huyo aliyekuwa akiamini ni mama yake mzazi, kumbe mama yake mzazi alifariki kitambo sana wakati yeye akiwa bado kinda.

Q Chilla anasema alipata ujasiri wa kusafiri na mwili wa mzazi wake huyo hadi Tanzania huku akijua kuwa safari yake ya maisha matamu yaliyojaa furaha ndio imefika ukingoni.

Msanii huyo anasema alikuwa akiishi na mama yake mkubwa huko Botswana ambapo, mama huyo aliyemlea kwa mapenzi tele na kumdekeza sana, alifariki dunia na kukatisha ndoto nyingi za Q-Chillah.

“Hadi anafariki mama yangu huyo mkubwa, nilikuwa nikiamini ndiye mama mzazi kwa vile mama yangu alifariki nikiwa mchanga.

“Wakati ninarudi na mwili wa mama, akili yangu ilikuwa timamu na nilijua kabisa sasa ninarudi jumla Tanzania na ndio mwanzo wa kukabiliana na maisha mapya na magumu sana,” anasema.

MAISHA YA SINEMA

Q Chilla anasema mama yake huyo alimdekeza mno na kumfanya ajione yeye ndiye yeye, lakini kifo chake kilimpa machungu yasiyofutika maisha mwake mpaka sasa.

“Katika malezi yake, mama yangu huyo alinidekeza sana, nilihama shule kadri nilivyotaka, nilipata kila nilichotaka. Kifo chake kilikuwa pigo kubwa sana kwangu.”

Q Chillah alifunguka kila jambo kuhusu maisha yake, mengine yakiwa ndio anayaweka hadharani kwa mara ya kwanza. Asilimia 80 ya maisha ya Q Chillah ni sinema tupu, ni safari iliyojaa maporomoko ya kimaisha yaliyoandamana na huzuni nyingi.

Hata safari yake ya kimuziki haitofautiani na masahibu yaliyomzonga katika maisha yake ya kawaida. Kwa kifupi Chillah amepita kwenye mitihani mingi.

MATUMIZI YA DAWA

Anasema kingine kinachomtia simanzi mpaka sasa ni kitendo cha kuingia kwenye matumizi ya dawa za kulevya kabla ya kuja kuacha baada ya bintie kumuelezea adha anayopata shuleni.

“Nilijiuliza kwa nini namtesa mwanangu kwa kitu kisicho na faida, nikala kiapo kuachana na ‘unga’ na ninashukuru kwa sasa nimezaliwa upya, japo kila nikikumbuka namna nilivyotaka kupoteza nakosa amani,” anasema Q Chilla anayetamba kwenye anga la muziki na nyimbo mbalimbali kali.

KAZI ZAKE

Mkali huyo anakumbukwa alivyoibuka mwanzoni mwa miaka ya 2000 na wimbo wa ‘Si Ulinikataa’ uliombeba na ambao ulielezwa kuwa ulikuwa ukipeleka ujumbe kwa mzazi wake wa kiume.

Baada ya kazi hiyo Q Chilla kipindi hicho akifahamika kama Q Chief aliendelea kusumbua na kazi mbalimbali zilizowafanya mashabiki kumzimikia na hata kuwa chimbuko la wakali waliokuja nyuma kwa kuiga sauti yake.

Diamond Platnumz amewahi kukiri kwamba, Q Chilla ni moja ya wasanii waliomtia ndimu na kumfanya ajitose kwenye muziki wa kizazi kipya na mpaka sasa anamkubali kinomanoma kwa utamu wa sauti yake.

KALI ZAIDI 50

Ukiachana Si Ulinikataa, Q Chilla ana ngoma nyingine kali zaidi ambapo zinafikia 50.

Baadhi ni; Kama Zamani, Kama Yule, Ninachokipata, Mariam, Nikilala Naota, Aseme, Umaskini Wangu, Carolina Mpenzi, Machozi, Nitampata Wapi, Penzi ni Nini,  Waiper, My Boo, Tutaonana Wabaya na Hicho Kiuno.

Pia kuna Yale Mapenzi, Ungeniumiza, Moyo Umechoka, Ntaanzaje, Ya Jana, Ugomvi wa Nini, Tunatawala, Nakuwaza, Dancing Floor, Adhabu Uliyonipa na Uhali Gani, mbali na kazi mpya za hivi karibuni baada ya kurudi upya.

Huyu ndio Q Chillah, ambaye kwa sasa ni tofauti kabisa na amekuwa mstari wa mbele kuwapa nasaha chipukizi.