Mkali wa Kiumeni achaneni naye

Muktasari:

Hata hivyo mwanadada Amtu Mandoza ‘Miss Mandoza’ ameweza kushangaza baada ya kuibuka kidedea katika ushiriki wa filamu inayotamba ndani na nje ya nchi, Kiumeni.

       KATIKA Bongo Movie ni ngumu msanii asiyefahamika kupata nafasi ya kuwa kinara wa filamu, hata awe na kipaji vipi.

Hata hivyo mwanadada Amtu Mandoza ‘Miss Mandoza’ ameweza kushangaza baada ya kuibuka kidedea katika ushiriki wa filamu inayotamba ndani na nje ya nchi, Kiumeni.

Msomi huyo wa Chuo Kikuu aliwafunika washiriki wengine waliojitokeza kuwania ushiriki wa filamu hiyo kiasi cha kushangaza wengi.

Hii ni kwa sababu imezoeleka waigizaji wengi ni Mamiss au wasanii wanaofahamika mbele ya watayarishaji na waongozaji wa filamu, tofauti na ilivyombamba Mandoza.

Mwanadada huyo aliyewahi kushiriki tangazo la shindano ya Bongo Star Search ‘Fungua Njia’ 2011 lililotengenezwa India, aliwashinda wenzake kama utani kutokana na kipaji kikubwa alichonacho katika uigizaji na kujiamini kwake mbele ya kamera.

KICHWANI ZIMO

Mandoza anayekiri filamu ya Kiumeni ni ya kwanza kwake, kitaaluma ni Msomi wa Mawasiliano ya Umma akiwa na Shahada ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Anasema tangu utotoni alikuwa na kiu ya kuja kuwa mwigizaji, lakini aliyapenda zaidi masomo kwa kuamini dunia ya sasa bila kuwa na elimu ya kutosha ni mtihani mkubwa.

Hata hivyo kutokana na ushawishi na kuvutiwa na mtayarishaji wa filamu wa kimataifa, Ernest Napoleon kupitia kazi zake kama Going Bongo, alijikuta akihamisha makali taratibu hasa baada ya kumaliza masomo.

Anasema kutua kwake kwenye filamu ya Kiumeni kulimpa presha, lakini aliweza kupita kwenye usaili kwa kipaji kilichofichika nyuma yake na uwezo wa kukariri muswada mara alipopewa na kuulizwa maswali.

“Nilikua na mashaka na maswali mengi, so nilienda tu kama kujifurahisha, waliponifanyia screening na script reading wakaona nafaa na mwishowe nimekuwa kiongozi wa Kiumeni,” anasema.

AIUMA SIKIO SERIKALI

Mwanadada huyo anaiomba serikali kutoa nafasi kwa sinema na kuipa nafasi sekta ya filamu kwani ameona thamani kubwa kutoka nje akitolea mfano Kenya kwa watayarishaji walivyoposti trailer na kutoa mwaliko kwa timu nzima ya Kiumeni kwenda Mombasa kuitambulisha.

“Serikali ya Kenya kupitia bodi ya filamu ya Kenya walipoona tu trailer walituita wakati mwamko kama huo Tanzania haupo, Wakenya wanajivunia sana Kiswahili na kujali kila sekta kwa kutambua inatoa hamasa kwa vijana kujiajiri.”

Anasema anashangaa serikali ya Tanzania kuchukulia poa sanaa ambayo ni njia nzuri ya kutangaza nchi na vivutio vyake sambamba na kuliingizia taifa pato kubwa.

KUMBE MTANGAZAJI

Kabla ya kuibukia kwenye filamu, Mandoza aliwahi kuwa mtayarishaji na mtangazaji wa Kipindi cha So So Fresh kilichokuwa kikiruka Clouds FM na kusaidia kuibua vipaji mbalimbali kama kina Young Killer, NayLee, Ruby na wengine kupitia msako wa vipaji wa Fiesta Super unaoendelea mpaka leo kuwaibua wengine.

Anasema Tanzania ina vijana wengi wenye vipaji wanaohitaji kupigwa tafu watoke walikojificha, kitu ambacho anaamini kinaweza kufanywa kwa ushirikiano wa wadau wa sanaa na serikali, japo anadai kuna dalili njema kwa utawala wa Awamu ya Tano.

YUPO SINGO BWANA

Amtu Mandoza anafichua kuwa bado hajaolewa na anaomba kila siku Mungu amjalie apate mwenza ambaye atajali na kuithamini kazi yake, ili kukwepa changamoto wanayokutana wasanii wenzake wa kike kuzuiwa kufanya kazi zao.

“Nasali kila siku Mungu anipe utashi kupata mtu atakayekua mume na mwenza wangu ambaye hataiona kazi yangu kuwa ni kikwazo, bali anipe sapoti ya kutosha kuendeleza kipaji changu,” anasema.

LUPITA AMPA MZUKA

Mandoza anasema mafanikio aliyonayo mwanamitindo na mwigizaji Mkenya anayeishi Marekani, Lupita Nyong’o, yanampa mzuka na kutamani kufika anga za kimataifa kwa kuamini hakuna kisichowezekana, mradi nguvu na uhai upo kwa msaada wa Mungu.

“Matarajio yangu nifike mbali zaidi na kuitangaza Tanzania nje ya mipaka kama afanyavyo Lupita anavyoitangaza Kenya nchini Marekani na kwingineko. Naamini nina uwezo wa kufanya hivyo,” anasema.

Anasema kikubwa anachoomba kwa sasa kuweza kupata ama kufanya kazi na kampuni yenye uwezo wa kufanya kazi kwa kiwango cha kimataifa kama ya

Afrika Kusini.

“Tunataka Lupita mwingine atoke Tanzania kwani mtaji wetu wa Lugha ya Kiswahili tukiutumia vema milango ipo wazi kufika mbali zaidi hapa, bado tupo mwanzoni kabisa,” anasema Mandoza anayewataka wasanii hasa wa kike kujiheshimu.