Kumbe tatizo ni Kanumba

Muktasari:

Hata baadhi ya wasanii wa tasnia hiyo wenyewe wamegawanyika pia, kuna wanaamini ndio basi tena na wengine wakisema bado inaendelea kudunda ila, lipo tatizo na kuzinyooshea vidole kazi za nje kuwa ndio tatizo linalowakwaza.

KWA muda mrefu sasa kumekuwa na mijadala kwenye mitandao ya kijamii na hata katika vinywa vya mashabiki wa filamu za Kitanzania wakibishana kuhusu tasnia ya Bongo Movie, wapo wanaoamini imekufa na wengine kupinga jambo hilo.

Hata baadhi ya wasanii wa tasnia hiyo wenyewe wamegawanyika pia, kuna wanaamini ndio basi tena na wengine wakisema bado inaendelea kudunda ila, lipo tatizo na kuzinyooshea vidole kazi za nje kuwa ndio tatizo linalowakwaza.

Ndio maana haikushangaza hivi karibuni, baadhi ya wasanii walifikia hatua ya kuandamana katika barabara kadhaa za jijini Dar es Salaam kuonyesha msimamo wao wa kupinga kazi za nje wakiamini ndizo zinazoua soko la kazi zao.

Mwanaspoti ambalo ni miongoni mwa wadau wakubwa wa tasnia hiyo, liliamua kumfungia safari mmoja ya nyota wa filamu Tanzania ambaye enzi za uhai wa Steven Kanumba walikuwa wakichuana na kufanya soko la tasnia hiyo kusimama imara kwelikweli.

Vincent Kigosi ‘Ray’ ndiye aliyezukiwa maskani kwake jijini Dar es Salaam na kufanyiwa mahojiano maalumu juu ya ukweli uliopo kuhusiana na kuporomoka kwa soko la filamu Tanzania na kutaka kujua kama ni kweli ndio limekufa ama la.

Jamaa wala hakuvuga kitu, aliamua kufunguka ukweli kwa mtazamo wake, tatizo ni nini na kitu gani kifanyike, mbali na kuzama kwenye historia ya maisha yake kwa ujumla kuanzia sanaa hadi ya kawaida na mipango yake. Hebu endelea naye....!

JAMAA MBISHI KINOMA

Ray ambaye alikuwa gumzo hivi karibuni kutokana na utani wake juu ya kudai weupe wake umetokana na kunywa maji mengi, kwanza anakataa kuwa sanaa ya filamu imekufa kama baadhi ya watu wanavyoamini.

Anasema tasnia hiyo haijafa, ila ni kweli imeyumba kutokana na hali ya maisha ilivyo na miundo mbinu inayochangia mambo kujitofautisha na miaka ya nyuma, ila anakiri soko kwa sasa halipo sawa.

“Tasnia ya filamu haijafa kama baadhi ya watu wanavyodai bali imeyumba na kuyumba ni kitu cha kawaida kabisa kwa binadamu kwani anaweza kuanguka na akasimama tena,” anasema.

Anasema kwa hali hiyo wao kama watayarishaji wakubwa wamekaa kimya wakijipanga na kuendeleza harakati ambazo zitainua tena soko lao na filamu kurudi katika ubora wao kama zamani pamoja na changamoto zinazojitokeza kwao ni kipindi cha mpito tu.

“Lazima tasnia itarudi kama awali, ni sawa tu na maisha ya mtu asiyekata tamaa katika kutafuta anapopata changamoto anajipanga na kurudi tena na sisi itakuwa hivyo tutarudi kama awali,” anasema.

“Napenda kuwaahidi Watanzania tupo katika kuandaa mapinduzi makubwa tutakaporudi lazima mtapata kazi nzuri sana zenye ubora wa hali ya juu.”

KUMBE TATIZO KANUMBA

Kumekuwa na madai kwamba kufariki kwa Kanumba ndio tatizo la kuyumba ama kufa kwa filamu Tanzania, jambo ambalo hata Ray anakiri kwa kusema kuwa, ni kweli kutokuwepo marehemu Kanumba ni tatizo la kuyumba kwa filamu Bongo.

Anasema pengo lake linaonekana wazi kwani kabla hajafa kulikuwa na ushindani mkubwa kati yake, lakini kwa sasa hakuna kitu kama hicho anahisi kama yupo pekee yake tu.

“Ni kweli kabisa, unajua Kanumba na Ray kama ilikuwa jina moja ukitaja Ray lazima utataja Kanumba, lakini mimi niseme hata leo nikifa mimi, JB au Dk. Cheni si rahisi pengo hilo kuzibika,” anasema.

“Hakuna mtu anayeweza kuziba pengo la Ray, JB au Dk. Cheni ujue kila mtu ana ladha yake katika kuigiza, ndio kama ilivyo kwa ndugu yangu Kanumba ukiongea unaweza kukufuru.”

KANUMBA BAB’ KUBWA

Anasema uwepo Kanumba enzi za uhai wake ulikuwa na faida kubwa kwake, kwani upinzani wao ulikuwa wa kimaendeleo.

Ray anasema kuwa kwa mfano Kanumba alikuwa akinunua vifaa vya uzalishaji filamu, naye ni lazima anunue, ilikuwa hivyo hivyo kwenye magari na maendeleo mengine yaliyochangia sanaa yao kukua na hata pato lao nalo kuwa juu.

“Tulikuwa tunashindana kweli kweli, kama akinunua gari la gharama, nami nitafanya hivyo ama kama nimeanza mimi, ilikuwa lazima naye afanye hivyo na hata kwenye kazi, akitengeneza filamu nzuri lazima nami nifanye hivyo kitu kilichotufanya tusibweteke na kuwa wabunifu kila uchao, yaani ilikuwa bab’kubwa,” anasema.

KWA SASA KWANI VIPI?

Ray hakatai kama kuna wasanii wazuri na wakali nchini kwa sasa, lakini anakiri kwamba hawapo kama ilivyokuwa kwa swahiba wake (Kanumba) anaamini waliopo sasa kazi yao kubwa ni kuigiza tu na sio watayarishaji.

Hilo limefanya hata ule ushindani uliokuwapo zamani ufifie, akiamini kuwa hana mshindani wa kweli anahisi kubaki pekee yake kwani kati ya watu wanaofanya filamu yupo pekee yake anayemiliki ofisi kwa ajili ya filamu.

Anaamini hata kuyumba kwa tasnia hiyo ya filamu kumechangiwa na kukosekana kwa ushindani tofauti na ilivyokuwa awali kati yake na marehemu Kanumba, kama ilivyo kwa muziki si rahisi kumzungmzia Ali Kiba bila ya Diamond.

“Hata katika soka ni vigumu kuizungumzia Yanga bila Simba ama kuipima Simba bila Yanga, ni timu zenye upinzani na ushindani wa karibu kuanzia kwa viongozi hadi mashabiki na ndivyo filamu ilitakiwa iendelee kama enzi za uhai wa Kanumba tulipokuwa tunachuana,” anasema.

Ray anaenda mbali kwa kutolea mfano upinzani na ushindani wa timu za Hispania kati Real Madrid na Barcelona anasema ukimtaja Messi lazima umtaje Ronaldo, hivyo ndivyo ilivyokuwa nchini kati yake na Kanumba na Bongo Movie kutisha.

“Narudia tena wasieleweke vibaya, wasanii wazuri wapo lakini si wale wa kujenga upinzani na kuleta ushindani, namwombea kwa Mungu amweke pema peponi na ikiwezekana siku moja tukutane huko kwani sisi sote kifo ndio njia yetu.”

Ray anapobanwa zaidi kuhusu ubovu wa filamu nyingi sokoni kuwa ni tatizo la tasnia hiyo kuyumba unajua ametoa majibu gani?

Unataka kujua kasema nini kifanyike ili kurejesha heshima ya fani hiyo nchini kama zamani? Ungana naye keshokutwa Alhamisi.