Kiba, Vanessa wanoga na Chris Brown

NYOTA wa muziki wa kizazi kipya wa Tanzania, Ali Kiba na Vanessa Mdee ‘Vee Money’ walitumia vema fursa ya kutumbuiza kwenye onyesho la mkali wa hip hop kutoka Marekani, Chris Brown kukonga nyoyo za mashabiki.

Wasanii hao walikuwa miongoni mwa waliotumbuiza sambamba na Chris na hawakufanya makosa kwani burudani waliotoa iliwafanya mashabiki wa  mji wa Mombasa kutokalia viti kwa muda wote waliokuwa jukwaani na kuburudika na wikendi yao. Chris alisimamisha shughuli zote mjini hapa kutokana na shoo yake hiyo iliyoacha gumzo kubwa.

Mkali huyo maarufu kama Breezy alipiga shoo ya ‘kufa mtu’ kwa muda wa saa moja na dakika kumi mfululizo kwa mashabiki waliofurika kwenye

Uwanja wa Mombasa Gofl Club, kiasi cha watu kushikwa kukaa vitini.

KING KIBA NOMA

Mkali huyo aliyepwa dakika 10 kutumbuiza kwa kuwa shoo nzima ilikuwa na mchizi Chriss Brown, lakini katika muda aliopewa aliutendea haki kwa kumwaga burudani ya nguvu iliyowapagawisha mashabiki wa muziki.

Kitendo cha kutoa burudani ya kufa mtu, rafiki yake ya karibuni, Gavana wa Mombasa, Hassan Joho alimuomba kurejea tena jukwani kupiga shoo baada ya Brown kumaliza kufanya yake.

Alipopanda kwa mara ya kwanza kwa mapenzi ya mashabiki wake, King Kiba aliiteka shoo hiyo kwa kishindo alipopiga ‘MacMuga’ muda tu alipokanyaga steji hiyo.

Wimbo wake wa ‘Aje’ nao uliwateka mashabiki hao na kuwaacha wakipiga kelele za furaha na kupata fursa ya kuchekechua pale alipowapa kibao chake  cha ‘Cheketa Chekutua’.

Kwa hakika Kiba alikongo nyoyo za mashabiki na kudhibitisha kuwa kweli ni mkali na anakijua anachokifanya jukwaani.

VEE MONEY ATIKISA

Mwanadada Vanessa Mdee akipanda jukwaani kwa mara ya kwanza kutumbuiza mjini Mombasa, alifunika mbaya kwa jinsi alivyopokewa kwa shangwe mara alipoitwa kutoa burudani.

Mwimbaji Bora huyo wa Kike wa Afrika, alichangamsha vema jukwaa kwa burudani nzito kupitia nyimbo zake alizoimba mfululizo za ‘Hawajui, ‘Come Over’ na ‘Niroge’.

Kwa namna mashabiki walivyopagawa ilithibitisha kuwa mwanadada huyo kweli anastahili tuzo aliyopewa hivi karibuni, kwani hakuwaangusha kwa burudani ya kimataifa aliyoimwaga uwanjani hapo.

CHRIS NDIO BALAA KABISA

Mkali wa hip hop, Chriss Brown aliyetua nchini hapa kwa ajili ya kutoa shoo hiyo iliyokuwa gumzo, kwa kweli aliwatendea haki mashabiki zaidi ya 2,000 walihudhuria onyesho hilo kubwa mpaka sasa ndani ya mwaka huu Kenya. Brown alipiga shoo ya uhakika kwa kuwaimbia nyimbo zake kali zinazotamba duniani kuanzia ‘Zero’, ‘Deuces’, ‘Don’t Judge Me’ na ‘Loyal’.

Jamaa hakuonekana kuchoka kwa namna alivyokuwa akijimwaga jukwaani kuangusha wimbo mmoja mpaka mwingine na kufanya mashabiki kuviacha viti vyao kwa muda ili kwenda naye sambamba.

 

MADEMU WAPAGAWA

Kwa namna mkali huyo wa Marekani alivyokuwa akimwaga burudani, ilifikia wakati mashabiki wa kike waliofurika kwa wingi kwenye onyesho hilo kupagawa.

Wengi wao walikuwa na hamu ya kuwa karibu na mkali huyo wa kimataifa, ila tu haikuwezekana kutokana na ulinzi mkali uliokuwapo katika shoo hiyo iliyobamba kinomanoma.

“Natamani ningepata shati yake ama nipate wasaa wa kuiba saa yake ya mkono kwa sababu ya upendo niliono kwa Chris brown. Nampenda mpaka  basi,” Ashley Wakesho, mmoja wa mashabiki waliopagawa na shoo alisikika.

WIZKID NAYE WAMO

Mkali mwingine wa Afrika kutoka Nigeria, Wizkid alikuwapo katika kunogesha burudani ya onyesho hilo akitumbuiza jukwaaa moja na Brown.

Wizkid anayejulikana pia kwa jina la ‘Star Boy’ alitumbuiza kwa dakika 25 ambazo alitumia kuimba nyimbo zake kali kiasi cha kuonekana kama anataka kumfunika Brown. Nyimbo zilizowatia wazimu mashabiki na kuimba naye sambamba ni pamoja na; ‘Caro’ na ‘Ojuelegba’.

 WABONGO KIBAO

 Siku hiyo Watanzania kibao walihudhuria onyesho. Wengi wao walitoka mikoa ambayo inapakana na Kenya. Hata hivyo Wagosi wa Kaya (wa Tanga) ndio walimiminika kwa wingi kwa kuwa Mombasa na Tanga ni pua na mdomo.