Hii ndiyo siri ya Genivieve kuwa juu siku zote

Tuesday April 23 2013Mwigizaji Genevieve Nnaji

Mwigizaji Genevieve Nnaji 

By new

LAGOS, NIGERIA LICHA ya urembo alionao, mwigizaji Genevieve Nnaji, amekuwa akishirikiana vizuri kimawasiliano na mashabiki wake hususani katika mitandao ya kijamii. Kwa kawaida mawasiliano hayo huchangia kuwaweka mastaa karibu zaidi na mashabiki wao. Haya ni baadhi ya mambo ambayo mashabiki wa Genevieve wameyataja kuwa ndiyo hasa yanawafurahisha kwake kiasi cha kumwona yuko juu siku zote. Ana kipaji cha kipekee Ana kipaji cha kipekee na hiyo ndiyo sababu iliyomfanya Oprah Winfrey alipofanya mahojiano naye katika shoo yake, kumwelezea kama Julia Robert wa Afrika. Kutokana na ukweli kwamba aliingia kwenye uigizaji akiwa na umri mdogo, Genevieve, hakusita kuudhihirishia umma kuwa habahatishi na badala yake amekuwa akikuza kipaji hicho siku hadi siku. Mafanikio hayo sasa yanamtambulisha kuwa ni mwanamke mwenye heshima kubwa na anayehitajika na kila prodyuza kwa ajili ya kufanya naye kazi. Filamu yake ya kwanza aliyoicheza kwa ustadi mkubwa na iliyoanza kumngíarisha inaitwa ëIjeí. Baada ya hiyo mambo yakawa yanaongezeka kila siku hadi kufikia filamu 300 alizoigiza hadi sasa. Anajua wajibu wake Waigizaji wengi hawaelewi ni nini maana hasa ya kuwa staa. Lakini kwa Genevieve mambo ni tofauti. Akiwa staa ameweza kupita katika changamoto kadhaa. Kutokana na umahiri alionao, amepambana na changamoto hizo huku akijifunza ni jinsi gani anaweza kuishi katika jamii. Hii inaelezwa kuwa ndio hasa sababu kubwa inayochangia mrembo huyu kujizolea mamilioni ya mashabiki. Muonekano mzuri, kujishusha kwa watu ni baadhi ya vitu vichache tu unavyoweza kuvigundua pindi unapozungumza naye. Siku zote amekuwa akionekana kama mfano mzuri wa kuigwa si tu na wasanii wenzake, bali hata na wanawake kwa ujumla. Pamoja na kwamba majarida mengi ya udaku yamekuwa yakimuandama kwa habari nyingi za uzushi, Genevieve amekuwa akisimama imara kutokana na ukweli kwamba amekuwa akifahamu ni nini hasa anawajibika nacho katika jamii. Si siri kukua kwa Nollywood kumechangiwa kwa kiasi kikubwa sana na uwepo wa waigizaji mahiri kama Genevieve. Ana mvuto wa kibiashara Tasnia ya burudani iko wazi kabisa kibiashara ambapo waliopo ndani yake hupambana kushinda vinginevyo hupotea. Haitoshi tu kuingia katika tasnia hiyo, kinachozingatiwa ni kuweza kudumu na kusimama kwa muda mrefu ili kujijengea heshima na kukubalika. Genevieve ameweza kufanya hivyo akihimili mikiki yote na kusimama vyema katika biashara ya uigizaji. Amekua akitumia uwezo wote kuhakikisha anashikilia nafasi yake. Alipoanzisha mtindo wake wa uvaaji, wasichana wengi walipenda kuvaa kama yeye, jambo hilo ndilo lililomtia moyo na hata kuanzisha kampuni yake ya mavazi inayofahamika kwa jina la St. Genevieve. Pamoja na kutojikita katika biashara ya utengenezaji filamu tofauti na ilivyo kwa waigizaji wenzake, Genevieve, ameweza kutumia taaluma yake ya Mahusiano ya Umma aliyoisomea nchini Uingereza katika kujiimarisha zaidi katika biashara zake mbalimbali. Kujituma na utayari Hili ndilo eneo ambalo mastaa wengi hususani waigizaji huboronga. Genevieve amekuwa akijituma sana katika kazi yake ya uigizaji filamu. Wakati wote ameonyesha utayari wake katika kufanya kazi, yuko makini kila siku. Kutokana na hili, si ajabu kumuona muigizaji huyu akiwa na idadi kubwa ya mashabiki ndani na nje ya Nollywood. Amekuwa akitoa sapoti kubwa kwa mashabiki wake. Siku zote amekuwa hataki kabisa kuwaangusha mashabiki wake. Ni picha ya kweli ya mwanamke wa Kinigeria. Anajua watu wanataka nini Kuwa juu katika tasnia yoyote ile hutegemea na jinsi staa husika anavyoipokea kazi yake yeye binafsi. Ikiwa ataichukulia kazi yake kiumakini zaidi iwe ni katika suala la kibiashara au wakati mwingine hata kijamii, hapo ndipo staa ataweza kuwa na nguvu siku zote. Hii ndio sababu nyingine iliyoweza kumweka Genevieve pale alipo. Amekuwa akichanganyika na watu wa aina mbalimbali pale anapohitajika. Pia amekuwa akiwajibika kwa kila jambo linalomhusu kwa wakati wake. Hadi pale staa atakapoamua kufanya kazi yake kama sehemu ya maisha yake, ndipo atakapoweza kupanda juu kwa urahisi. Genevieve anasimama akiwa na sifa kibao; ni mama, mke, ni mkurugenzi, ni mwanamitindo, ni mwalimu na pia ni mwanaharakati katika maendeleo ya mwanamke mweusi.