Jeuri ya pesa ya wasanii wa filamu Bongo

Tuesday April 23 2013Wema Sepetu

Wema Sepetu 

By new

JULIETH KULANGWA MATANUZI ni sehemu ya maisha ya mastaa wengi duniani kwani huchukuliwa kuwa ndiyo kipimo cha mafanikio. Lakini pia ukishafanikiwa, maisha lazima yabadilike. Huko Hollywood kila siku tunasoma habari za watu maarufu kununua magari ya kifahari ambayo mengine thamani yake unaweza kujenga shule nane za msingi zenye maabara na vitabu vya kutosha katika nchi yoyote ya Afrika Mashariki. Ingawa Afrika bado sanaa hailipi kwa kiwango hicho, lakini wasanii wetu wamekaza msuli kuonyesha jeuri ya pesa. Mbali ya sanaa, wasanii hao wamekuwa na kazi nyingine ambazo zimekuwa zikiwaingizia kipato. Kazi hizo ni kama vile kufanya matangazo, matamasha na biashara zao binafsi. Stori ya Wema Sepetu kutoa milioni 13 kwa ajili ya kumwokoa na kifungo, msanii mwenzake wa filamu za Bongo, Kajala Masanja, bado haijasahaulika pamoja na kuwa wengi wamempongeza kwa kitendo hicho. Hata hivyo wema wake huo umemwingiza katika rekodi ya mastaa wenye fedha na matanauzi Bongo. Alifanya kitendo hicho miezi michache baada ya kuagiza gari la aina ya Audi Q7 ambalo mpaka lianze kutumika Bongo lazima zimtoke si chini ya Sh70 milioni za Kitanzania. Lakini ikumbukwe pia mwishoni mwa mwaka jana, Wema alionyesha nyumba yake ya kifahari iliyopo Kijitonyama jijini Dar es Salaam. Mpaka kukamilika nyumba hiyo iligharimu Sh270 milioni. Ni wasanii wachache wa muziki wa kizazi kipya wa Bongo wanaomiliki nyumba za kifahari ambazo tumewahi kuziona. Wasanii hao ni Lady Jay Dee na Profesa Jay, lakini hao ni wakongwe kwa Wema ingawa anakula nao sahani moja. Wakati Wema akiendelea kupamba vichwa vya habari, lipo tukio jingine lililowahi kufanywa na staa wa Bongo Movie, Jackline Wolper ambaye alijitolea dola za Marekani 1,000 kwa ajili ya kuchangia matibabu ya marehemu, Juma Kilowoko 'Sajuki' kama alivyokuwa akifahamika na wengi. Pamoja na kutoa fedha hizo, Wolper naye ameripotiwa kumiliki gari la kifahari aina ya BMW X6 ambalo nalo linagharimu Sh170 milioni za Tanzania. Mrembo mwingine aliyewahi kupamba video za wasanii mbalimbali Bongo ni Jackline Patrick 'Boss Lady'. Naye hayuko nyuma katika kuonyesha jeuri ya fedha, anaishi katika jumba la kifahari lililoko Mbezi Beach. Naye anasukuma gari ya kifahari aina ya Benz ambalo kulimiliki unahitaji kuwa na mfuko uliotuna. Ukweli unabaki kuwa waasisi wa mashindano na kujionyesha kwenye tasnia hii ni Vicent Kigosi 'Ray' na marehemu Steven Kanumba ambao walikuwa wakifanya hivi kwa kushindana na mwisho wa siku ikawa ndio utamaduni wao. Safari ya Ray na Kanumba kumiliki majina makubwa na mwisho mali ilianza mbali, walianza kwa kushindana nani ni bora katika uigizaji, mwishowe kila mmoja akaanza kujigamba kwa kile alichovuna kutokana na kazi hiyo. Stori inaanza baada ya mastaa hao kwa kujigamba mmoja akijiita 'The Great' na mwingine 'The Greatest', maneno haya yaliandikwa nyuma ya magari aina ya Escudo ambayo kila mmoja likuwa akimiliki. Baadaye wakabadilisha magari na kukaa katika Harrier na baadaye Land Cruiser kabla ya Kanumba kukutwa na mauti mwaka jana.