Malkia wa Kwetu Pazuri aibuka kivingine

Tuesday April 2 2013

By new

JAMES MAGAI MWIMBAJI maarufu wa kwaya ya Ambassadors of Christ ya Kanisa la Waadventista wa Sabato la mjini Kigali, Rwanda, Yvonne Umulisa, ameibuka tena katika albamu mpya ya kwaya hiyo baada ya kukosekana katika matoleo matatu mfululizo. Umulisa ambaye alitamba na wimbo wa ‘Kwetu Pazuri’ akiwa mwimbaji mwanzilishi na kujipatia umaarufu mkubwa, aliondoka katika kwaya hiyo kwa muda baada ya kufunga ndoa miezi michache baada ya kunusurika katika ajali ya gari. Baada ya kukosekana katika albamu tatu za kwaya hiyo, hatimaye ameibuka tena katika albamu mpya namba 8 iitwayo ‘Kaeni Macho’. Katika albamu hiyo, Umulisa anatamba na wimbo ‘Twawona Okuswala’ (Tumeepushwa Aibu), wimbo huo umeimbwa kwa lugha ya Kiganda. Katika wimbo huo unaoanza kwa kibwagizo, Umulisa anaonekana akiongoza kuimba ubeti wa kwanza kwa hisia kali na kwa umahiri mkubwa akitoa sauti yenye mvuto kama alivyoimba katika wimbo wa Kwetu Pazuri. Umulisa aliliambia Mwanaspoti akiwa Kigali kuwa anajisikia furaha sana kurejea katika kwaya yake hiyo na kuungana tena na mashahabiki wake kupitia huduma ya uimbaji. Kuhusu siri ya kuendelea kufanya vizuri katika uimbaji kwenye albamu hiyo alisema: "Mimi napenda sana kuimba, hivyo ninafanya kitu ninachokipenda. Siwezi kujua kiwango changu kikoje, ila wasikilizaji ndio wanaweza kujua." Akizungumzia kiwango cha mwimbaji huyo baada ya kurejea tena katika huduma hiyo, Mwalimu wake, Ssozi Joramu, alisema kuwa Umulisa ni balaa. "Yule dada ni balaa. Inashangaza, mtu aliyekaa muda wote ule bila mazoezi lakini hajapoteza kiwango,"alisema Ssozi. Umulisa aliachana na kwaya hiyo kwa muda alipofunga ndoa miezi michache tu baada ya kunusurika katika ajali ya gari iliyolikumba kundi hilo wakati wakirejea kwao kutoka Dar es Salaam, ilikuwa Mei 9, 2011. Waimbaji wenzake watatu walifariki dunia na wengine kadhaa wakajeruhiwa vibaya. Aliolewa mjini Gisenyi huko kwao jambo lililomfanya asimame kwa muda kuimbia kwaya hiyo. Sasa amehamia tena Kigali na mumewe. Pia hakuweza kushiriki katika matoleo matatu ya albamu za kwaya hiyo yaliyofautia, wala katika safari za kwaya hiyo zilizofuatia, jambo lililowafanya mashahabiki wake waliokuwa na hamu ya kumuona waulize maswali mengi.