Cheki Ney wa Mitego alivyodakwa

Muktasari:

Jeshi la Polisi limethibitisha kumkamata Wa Mitego ambaye wimbo wake huo alioutoa siku tano zilizopita umejipatia umaarufu mkubwa kwenye mitandao ya kijamii.

STAA wa muziki wa hip hop mwenye tungo tata, Ney wa Mitego juzi Jumamosi amekamatwa na polisi saa chache baada ya kumaliza kupiga shoo yake Turiani mjini Morogoro.

Wa Mitego ambaye Julai 27, mwaka jana aliitwa kituo kikuu cha Polisi kutokana na tungo zake tata, juzi alinaswa usiku ikiwa ni siku tatu tu tangu aanze kusakwa na polisi kutokana na kutoa wimbo tata wa ‘Wapo’.

Jeshi la Polisi limethibitisha kumkamata Wa Mitego ambaye wimbo wake huo alioutoa siku tano zilizopita umejipatia umaarufu mkubwa kwenye mitandao ya kijamii.

Rapa huyo alikamatwa Turiani, Mvomero na kupelekwa  kituo cha Polisi Dakawa kabla ya kupelekwa kituo cha Morogoro mjini na kisha kusafirishwa mpaka kwa Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Dar es Salaam.

Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Jeshi la Polisi na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Ulrich Matei alithibitisha kumkamata rapa huyo. 

“Alikamatwa saa nane usiku wa leo (jana), kwa kosa la kutoa wimbo wenye maneno ya kashfa dhidi ya Serikali na shauri lake lipo Dar es Salaam, atapelekwa kuhojiwa kuhusu masuala yake ya kazi kwa Mkuu wa Upelelezi Mkoa,” alisema Kamanda Matei.

“Tayari amefikishwa kituoni na tupo katika mchakato wa kuwasiliana na wenzetu wamchukue, aende anakohitajika,” alisema Kamanda Matei. Rais wa Shirikisho la Muziki Tanzania, Ado Novemba alisema amepokea taarifa kwa mshtuko ila akasisitiza wasanii waimbe nyimbo zenye maadili.