Bocco awahishwa Dar kutibiwa

Muktasari:

  • Bocco aliumia dakika ya 32 baada ya kuifungia timu yake bao la uongozi dhidi ya Mwadui FC juzi Alhamisi na kushindwa kuendelea na mchezo huo uliomalizika kwa sare ya mabao 2-2 mjini Shinyanga.

SIMBA imeshtushwa na majeraha aliyoyapata straika wake, John Bocco, hivyo kufanya juhudi za mapema ili kuhakikisha anafanyiwa kipimo kikubwa cha MRI kutambua uzito wa tatizo lake, ijapokuwa daktari wa timu hiyo, Yassin Gembe, amesisitiza ni tatizo dogo tu.

Bocco aliumia dakika ya 32 baada ya kuifungia timu yake bao la uongozi dhidi ya Mwadui FC juzi Alhamisi na kushindwa kuendelea na mchezo huo uliomalizika kwa sare ya mabao 2-2 mjini Shinyanga.

Daktari Gembe ameliambia Mwanaspoti kuwa Bocco anaendelea vyema, lakini uhakika kwamba atarejea lini uwanjani ni baada ya kufanyiwa vipimo vikubwa.

“Huku amepata matibabu ya awali ambayo hayawezi kutueleza ukubwa wa tatizo, hivyo ni lazima afanyiwe kipimo kikubwa cha MRI ili kujua ukubwa wa tatizo na litamweka nje kwa muda gani,” alisema.

“Anaendelea vizuri tofauti na jana (juzi) alipoumia, hivyo akifika tu Dar es Salaam anaenda kufanya kipimo moja kwa moja ndipo tutajua kila kitu.”

Simba ilirejea jana Ijumaa usiku ambapo kesho Jumapili itaondoka kwenda Djibouti kwenye mechi ya marudiano ya raundi ya awali ya Kombe la Shirikisho barani Afrika dhidi ya Gendarmerie.

Katika mchezo wa kwanza Wekundu wa Msimbazi walishinda hapa nyumbani mabao 4-0.