Bocco, Okwi kiulaiiini!

Muktasari:

  • Wawakilishi hao wanakabiliwa na mechi ngumu dhidi ya Al Masry ya Misri katika mechi mbili za raundi ya kwanza ya Kombe la Shirikisho.

SIMBA ina dakika 180 za kuamua hatma yao katika ushiriki wao wa michuano ya kimataifa.

Wawakilishi hao wanakabiliwa na mechi ngumu dhidi ya Al Masry ya Misri katika mechi mbili za raundi ya kwanza ya Kombe la Shirikisho.

Kama hesabu zao zitakataa ndani ya muda huo, pengine mikwaju ya penalti itaamua hatma yao mbele ya Waarabu kwa sababu ni lazima mshindi baina yao apatikane ili moja isonge mbele na nyingine iage mashindano.

Tayari Simba imejiaminisha lazima Mwarabu apigwe nje ndani ili iingie kwenye hatua ya mwisho ya kuwania kuingia makundi ya shirikisho na kufuata nyayo za watani zao, Yanga waliowahi kuiweka mwaka 2016.

Hata hivyo, nahodha na nyota wa zamani wa kimataifa wa Msimbazi, aliyewahi pia kung’ara na timu za Mtibwa Sugar, JKT Ruvu na Taifa Stars, Mussa Hassan Mgosi, amekiangalia kikosi cha Simba na kuifuatilia Al Masry akajikuta akitasabamu.

Unajua kwa nini? Amegundua, Simba ina kikosi kitamu na chenye wachezaji wanaoweza kuwapa raha mashabiki wa Msimbazi.

Mgosi aliwaangalia Shiza Kichuya, Emmanuel Okwi, Asante Kwasi, Erasto Nyoni, Aishi Manula, John Bocco na nyota wengine wa kikosi cha msimu huu chini ya Kocha mzoefu wa mechi za kimataifa, Mfaransa Pierre Lechantre na kujikuta akichekelea.

Mgosi alisema ni kweli soka halichezwi kwa rekodi ama historia, bali ni namna timu itakavyoandaliwa, hivyo anaamini kama nyota wa Simba wataandaliwa vyema na kutekeleza majukumu yao kwa kujituma uwanjani katika mechi zao za Al Masry, Wamisri lazima watakufa mbele ya Aristide Bance na Ahmed Gomaa wao.

MSIKIENI

Mgosi alisema kama ambavyo Simba walivyoshtuka kusikia watakutana na Al Masry ndivo ambavyo Wamisri nao wameshtuka kwa kutambua Simba sio timu ndogo na pengine wanafanya maandalizi ya kuhakikisha wanapata matokeo mazuri.

“Hivyo nisema tu, wachezaji wa Simba wakiandaliwa vyema na wao wenyewe wakajua thamani ya jezi ya klabu yao na kitu gani ambacho watu wanaowazunguka kwa maana ya wanachama na mashabiki wanataka nini, wataibeba timu,” alisema.

Mgosi alisema kwa aina wachezaji waliopo Simba na jinsi wanavyoibeba timu kwa sasa katika Ligi Kuu Bara, ndivyo ambavyo anaamini hata katika mechi dhidi ya Al Masry ndivyo itakavyokuwa na kuwataka mashabiki wa Simba wasiwe na hofu.

“Naamini Simba wanapeta kwa Wamisri kwa sababu mechi hizo ndizo za kuamua hatma ya Msimbazi kuendelea ama kutoka, hivyo nyota wa Simba lazima waandaliwe mapema na viongozi kuelekea mechi hiyo.”

MZUKA SANA

Kocha Msaidizi wa Simba, Djuma Masudi ambaye akishirikiana na bosi wake, Pierre Lechantre wameiongoza Simba katika mechi nane za Ligi Kuu na zile za kimataifa kuvuna jumla ya mabao 21 na kufungwa mawili tu, anaamini Simba itapenya.

Kocha Djuma alisema anaamini vijana wake ambao kesho watakuwa na kibarua cha mechi ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Mbao, watapambana kuhakikisha Simba inavuka raundi ya kwanza bila kujali inacheza na timu ya aina gani.

“Tunajua kila tunapozidi kusonga mbele ndivyo tunavyokutana na ushindani mkali, tuna wachezaji nyota wanaojua kujitoa uwanjani, kwa nini tuwe na hofu, tunaamini hata Al Masry inafungika kwa sababu wachezaji wetu ni bora,” alisema Djuma.

Mgosi naye alisisitiza nyota wa Simba wazingatie maelekezo ya walimu wao na kuongeza juhudi zao ili kuweka historia nyingine ya kuwang’oa Wamisri kama ilivyokuwa 2003, Msimbazi walipoing’oa Zamalek waliokuwa watetezi wa CAF.

Katika mwaka huo Simba iliitungua Zamalek waliokuwa mabingwa watetezi wa Ligi ya Mabingwa Afrika kwa bao 1-0, kisha kwenda kupoteza kwa idadi kama hiyo nchini Misri kabla ya kupigiana penalti na Simba kushinda kuingia makundi.