Beki wa Yanga, Chama afariki kuzikwa kesho

Monday January 8 2018

Chama alipata umaarufu wakati akiitumikia Yanga

Chama alipata umaarufu wakati akiitumikia Yanga mwaka 1981 na ndipo alipobatizwa jina la Jogoo kwa umahiri wake. 

By Majuto Omary

Dar es Salaam. Mwili wa beki wa zamani wa klabu ya Yanga, Athumani Juma ‘Chama’ atazikwa kesho saa  7.00 mchana kwenye makaburi ya Kisutu jijini Dar es salaam.

Chama ambaye aliichezea Yanga miaka ya 80 na kujipatia umaarufu mkubwa, alifariki dunia usiku wa kuamkia leo, Jumatatu baada ya kulazwa kwa takribani wiki mbili kwenye hospitali ya Taifa ya Muhimbili akizusumbuliwa na maradhi ya kuharusi.

Msemaji wa familia, Abeid Mziba amesema kuwa  kwa sasa msiba upo nyumbani kwa marehemu, Yombo Dovya karibu na kituo cha daladala cha Abiola.

Mziba ambaye alicheza na marehemu Chama Yanga, alisema kuwa kuwa msiba huo ni pigo kubwa kwa mashabiki wa mpira wa miguu na hasa wanachama na mashabiki wa Yanga ambao mbali ya kumpachika jina la utani la Chama, pia walimpa jina lingine la ‘Jogoo’ kutokana na uchezaji wake akiwa Yanga na timu ya Taifa.

“Marehemu ameacha mke na watoto wawili, tunawaomba wadau wa soka na michezo kwa ujumla kumshiriki kuwapa faraja wafiwa katika kipindi hiki kigumu cha maombolezo na mazishi kwa ujumla,” alisema Mziba.

Athuman Chama Jogoo ni nani?

Alianza kucheza soka akiwa mdogo, mwenyewe anasema alipenda kucheza namba mbili na namba nne tangu akiwa na umri mdogo.

Akiwa mtoto wa kwanza kati ya watano kwenye familia yao, Chama alichezea timu mbalimbali kabla ya kujiunga na Pamba United ya Mwanza.

Chama alicheza Yanga kwa miaka zaidi ya 10 lakini wakati huo walicheza kwa mapenzi zaidi na walicheza kwa moyo ikilinganisha na wachezaji wa sasa.

Kikosi cha kwanza cha Yanga waliocheza na Chama miaka ya 1983 na 1985 ni; Joseph Fungo, Yusuf Bana, Ahmed Amasha ‘Mathematician’, Athumani Juma Chama ‘Jogoo’, Isihaka Hassan Chuku, Juma Mukambi ‘Jenerali’, Hussein Iddi, Charles Boniface Mkwasa, Abeid Mziba ‘JJ Masiga’, Elisha John na Ali Mchumila.

Pia walikuwepo; Makumbi Juma ‘Homa ya jiji’, Omari Hussein ‘Keegan’, Juma Kampala na wengine wengi.

Apachikwa jina la Jogoo

Wakati wa michuano ya Kombe la Chalenji mwaka 1981, kulikuwa na mchezaji mmoja wa Harambee Stars ya Kenya, Sammy Onyango ‘Jogoo’. Alikuwa makini sana katika ngome.

Alikuwa na uwezo wa kukabiliana na washambuliaji mbalimbali hasa katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Baada ya mashindano yale ya 1981 ambayo pia kulikuwa na mtu aliyekuwa akiitwa Ambroce Ayoi ‘Golden Boy’ wengi waliufananisha uwezo wa Sammy Onyango na Athumani Juma Chama na taratibu jina likafika kwa mwenyewe.

Chama na Mogella

Chama na Mogella…..Chama na Mogella. hii ni kumbukumbu ambayo Chama ameiacha kwenye soka la Tanzania wakiwazungumzia, aliyekuwa mshambuliaji wa Simba, Zamoyoni Mogella na beki huyo wa Yanga (Chama).

Itakumbukwa Yanga walitishika na soka ya Mogella katika moja ya mechi za watani, ndipo waliamua kumwekea ulinzi mkali, wa Athumani Juma Chama ambaye aliambiwa popote anapokwenda Mogella awe naye.

Chama alifanya kazi yake, basi ikawa kazi moja, Chama na Mogella kiasi cha Mogella kuumia na kufanyiwa huduma ya kwanza, Mogella alifunga bandeji mfano wa ‘lumundi’ kichwani na kurudi uwanjani, hata hivyo Mogella hakutikisa nyavu siku hiyo.

Maisha baada ya soka

Chama alistaafu soka mwaka 1990 baada ya kuitumikia Yanga kwa miaka 10.

Baada ya kustaafu aliendelea kufanya biashara zake ndogo ndogo kabla ya kuugua mwaka 2014 na kushindwa kufanya chochote hadi sasa.