Batshuayi amweka njia panda Conte

Monday February 12 2018

 

LONDON, ENGLAND. Kocha Antonio Conte anatafuta pa kuficha uso wake baada ya mashabiki wa Chelsea kutumia kurasa zao za mitandao ya kijamii kumshambulia Mtaliano huyo kwa kitendo cha kumwondoa mshambuliaji Michy Batshuayi.

Mshambuliaji huyo tangu alipotua Borussia Dortmund  amefunga mabao matatu katika mechi mbili baada ya kufunga tena juzi Jumamosi kwenye mechi ya Bundesliga dhidi ya Hamburg.

Mshambuliaji huyo aliyetolewa kwa mkopo kwenye dirisha lililopita, amehusika katika kila bao la Dortmund tangu alipojiunga na timu hiyo, jambo ambalo linamfanya Conte ajione wa ajabu kutokana na kumwondoa huko Stamford Bridge na kisha kumsajili Olivier Giroud kutoka Arsenal.

Batshuayi alihitaji kuchezeshwa ili kuwa fiti kwa ajili ya fainali zijazo za Kombe la Dunia, lakini kocha Conte aliona kwamba hafai kupata nafasi hiyo anayotaka jambo lililomfanya atimkie Dortmund kwa mkopo baada ya Wajerumani hao kumuuza Pierre-Emerick Aubameyang kwenda Arsenal kwa ada ya Pauni 60 milioni.

Baada ya kufunga mabao mawili katika mechi yake ya kwanza, Batshuayi akawapigia tena bao la kuongoza Dortmund dhidi ya Hamburg kabla ya Mario Gotze kupigilia msumali wa pili. Baada ya kufunga bao hilo, Batshuayi alishangilia kwa staili ya Aubameyang na kupiga sarakasi.