Barca yamweka Coutinho njiapanda

Muktasari:

Coutinho (25), amejiunga na Barcelona kwa Pauni 145 milioni na ametia saini mkataba wa miaka mitano hata hivyo atalazimika kukaa nje ya uwanja wa wiki tatu kabla ya kuanza kupigania namba katika kikosi hicho tofauti na ilivyokuwa Liverpool.

London, England. Uamuzi wa kiungo Philippe Coutinho kujiunga na Barcelona kwa sasa akitokea Liverpool umeweka njia panda nafasi yake ya kucheza Kombe la Dunia Russia mwaka huu.

Kiungo huyo mbali ya kuweka njia panda kucheza fainali za Russia pia amepoteza nafasi ya kucheza Ligi ya Mabingwa kwa mujibu wa kanuni za UEFA, kwa sababu tayari alishaicheza Liverpool katika mashindano hayo.

Coutinho (25), amejiunga na Barcelona kwa Pauni 145 milioni na ametia saini mkataba wa miaka mitano hata hivyo atalazimika kukaa nje ya uwanja wa wiki tatu kabla ya kuanza kupigania namba katika kikosi hicho tofauti na ilivyokuwa Liverpool.

Mapema leo Mbrazil huyo ameandika waraka mzito kwa mashabiki wa Liverpool akitoa sababu za kuondoka Anfield katika usajili wa dirisha dogo mwezi huu.

Coutinho alisema ndoto yake ilikuwa kucheza Barcelona kama ilivyokuwa kwa klabu hiyo wakati akitokea Inter Milan mwaka 2015 alipotua Liverpool kwa Pauni 8.5 milioni.

Kiungo huyo juzi alitambulishwa kwa mashabiki 7,000 waliokwenda Nou Camp, lakini atakuwa nje ya uwanja wiki tatu baada ya vipimo vya afya kubaini ana jeraha katika mguu.

“Nimeondoka Liverpool ili kutimiza ndoto yangu Barcelona, nilikuwa na ndoto kucheza Liverpool na nimetimiza na kudumu kwa miaka mitano,”alisema Coutinho.

Alisema alifanya kazi nzuri Liverpool, lakini anataka kwenda kupata uzoefu mpya Barcelona baada ya kuifungia timu hiyo mabao 54 katika mechi 201 alizocheza Anfield.

Licha ya kutambulishwa, Coutinho hajapewa jezi ingawa kuna uwezekano akapewa ‘uzi’ namba 14 uliokuwa ukivaliwa na nguli wa zamani wa Barcelona, Johan Cruyff.

Jezi namba 14 inavaliwa na beki nguli wa timu hiyo Javier Mascherano ambaye taarifa za awali zimedokeza huenda akapigwa bei katika usajili wa dirisha dogo mwezi huu.

Mchezaji huyo alitoa shukrani kwa mashabiki wa Liverpool kuumunga mkono katika miaka mitano aliyodumu Anfield.