Akili za Mfaransa zaibeba Simba

Muktasari:

Vinara hao wa Ligi Kuu Bara wanakwenda katika mchezo huo kusaka ushindi, baada ya kulazimishwa sare ya 2-2 kwenye mechi ya raundi ya kwanza.

SIMBA itakwea pipa kesho Jumatano kwenda Misri kumalizana na Al Masry katika mechi ya Kombe la Shirikisho Afrika, lakini akili aliyofanya kocha wa timu hiyo, Pierre Lechantre imerahisisha kazi kwa vijana wake kuwa nyepesi kabisa.

Vinara hao wa Ligi Kuu Bara wanakwenda katika mchezo huo kusaka ushindi, baada ya kulazimishwa sare ya 2-2 kwenye mechi ya raundi ya kwanza.

Hata hivyo, kabla ya kuondoka jijini Dar es Salaam, Simba ilikataa kucheza mechi zake mbili za ligi dhidi ya Mtibwa Sugar na Njombe Mji tena za ugenini kwa kile ilichodaiwa ni agizo la Lechantre hivyo, kuzusha kelele nyingi mtaani.

Lakini, Kocha Abdallah Kibadeni ‘King’ amefichua alichokifanya Mfaransa huyo kuigomea timu yake kucheza mechi za ligi kabla ya kuvaana na Al Masry, ilikuwa ni akili ya maana kwelikweli. Pia, kwa akili hiyo Simba inaweza kupata ushindi ugenini kwani, kama wangecheza ingweza kuwaletea madhara zaidi.

“Wanacheza mechi ngumu na muhimu na wameipa uzito mkubwa ndio maana wameomba muda wa kutosha ili kujiandaa. Hiyo inaweza kuwa na faida kubwa kwao kwa kupata muda wa kutosha,” alisema Kibadeni na kuongeza;

“Kikosi cha Simba ni kipana, lakini wachezaji wao mahiri ambao wanafanya vizuri msimu huu, wengi ni majeruhi labda waliogopa hilo wanaweza kuwapoteza kama wangeumia kabla ya mechi hiyo.

“Kama watafanya maandalizi muhimu ya kimwili na kiakili itakuwa faida kuwa tayari kupambana na kupata matokeo ambayo wanatarajia, lakini wakishindwa kufanya hivyo wanaweza kushuka morali.”

Naye nyota wa zamani wa timu hiyo, Boniface Pawasa alisema; “Utaratibu huu ulikuwepo muda mrefu kwa timu inapokuwa na ratiba ngumu za kimataifa na Simba inaweza kuwa na faida ya kupata muda wa kutosha wa kujiandaa tofauti kama wangecheza mechi za ligi,

“Wanasafiri umbali mrefu kwenda Misri na muda waliokuwa nao unatosha kabisa kusafiri mapema na kuzoea mazingira na kama kutakuwa na fitna watakabiliana nazo,” alisema.

Hata hivyo, alisema Simba inaweza kupata hasara ya kuwapunguzia morali wachezaji wao kwani, wanapaswa kuwa fiti muda wote kwa maana ya kucheza uwanjani.

“Kama wangecheza mechi za ligi na kushinda ingewaongezea morali na hata wakienda Misri wangekuwa moto, ila kocha ametumia akili kufanya maamuzi hayo,” alisema.

Lakini, Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ alikuwa na mtazamo tofauti kwa kusema; “Sidhani kama imefanya maamuzi sahihi, kwani itawaondolea ubora wachezaji kuelekea mchezo huo na wasishangae nyota wanaowategemea wakacheza vibaya dhidi ya Al Masry.

“Wanasema wanaogopa mastaa wao kuumia, hiyo ni mipango ya Mungu unaweza kuumia hata kama ukiwa nyumbani, hivyo Simba hawakuwa sahihi.”

Simba itakayokabiliana na Al Masrty kwenye mchezo huo, itaondoka nchini kesho Jumatano kabla ya Jumamosi kushuka Uwanja wa Port Said kuivaa Waarabu hao, ambao jana usiku walikuwa uwanjani kucheza mechi ya ligi ya nchi yao.