Ajibu apewa kazi maalumu

BENCHI la ufundi la Yanga, limemkabidhi kazi maalumu straika wake, Ibrahim Ajib kupiga mipira yote ya adhabu, kona pamoja na penalti.

Ajibu tayari amefunga mabao mawili kwa mipira ya adhabu, jambo ambalo limelivutia benchi la ufundi la klabu hiyo kuamua kumpa kazi hiyo.

Katika mchezo wa juzi Jumatano dhidi ya Mwadui FC, Ajib ndiye alikuwa mpigaji mkuu wa kona na faulo na moja kati ya pigo lake lilipanguliwa na kipa wa Mwadui na kugonga mtambaa wa panya.

Kocha msaidizi wa timu hiyo, Shadrack Nsajigwa alisema Ajib amepewa kazi hiyo ndio maana alikuwa anawajibika kila ilipokuwa ikitokea faulo ama kona kwenye mechi hiyo ya Mwadui

“Kona na faulo alizokuwa anapiga Ajib sio kwamba alijiamulia, bali yalikuwa ni maelekezo ya benchi la ufundi, ndio maana alikuwa shapu kutimiza wajibu wake,” alisema.

Katika hatua nyingine, Nsajigwa alisema walilazimika kumtumia staa wao, Amissi Tambwe kwa dakika 49 tu dhidi ya Mwadui kwa kuwa alikuwa ametoka kuugua homa kali na bado hajawa fiti kwa asilimia zote.

“Mchezaji ametoka kuumwa huwezi kuanza naye kwa kasi, muda aliotumika ulikuwa sahihi kwake na ndio uliopangwa acheze.Tambwe akiwa fiti zaidi ataisaidia Yanga,” alisema.

Tambwe raia wa Burundi  alikuwa  tegemeo katika safu ya ushambuliaji ya Yanga kwa kupachika mabao, awali alikuwa  na matatizo ya goti ambayo yalimuweka nje kwa muda mrefu. Mara ya kwanza kumtumia ilikuwa ni katika mechi ya Kombe la FA dhidi ya REHA.