Adhabu kwa waamuzi zitolewe mapema

Mwamuzi Martin Saanya.

Muktasari:

  • Saanya ambaye alikuwa mwamuzi wa kati amekuwa akilaumiwa kwa kitendo cha kukubali bao la mkono lililofungwa na Amissi Tambwe wa Yanga kisha kumwonyesha kadi nyekundu nahodha wa Simba, Jonas Mkude. Hata hivyo kadi hiyo ilifutwa siku nne baadaye.

KAMATI ya Waamuzi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) imewaondoa katika orodha ya Waamuzi, Martin Saanya na Samuel Mpenzu kwa kosa la kuchezesha mechi ya watani wa jadi Simba na Yanga chini ya kiwango.

Saanya ambaye alikuwa mwamuzi wa kati amekuwa akilaumiwa kwa kitendo cha kukubali bao la mkono lililofungwa na Amissi Tambwe wa Yanga kisha kumwonyesha kadi nyekundu nahodha wa Simba, Jonas Mkude. Hata hivyo kadi hiyo ilifutwa siku nne baadaye.

Katika mchezo huo Mpenzu alilaumiwa kwa kosa la kuonyesha kuwa mshambuliaji wa Simba, Ibrahim Ajibu alikuwa ameotea wakati hakuwa amefanya hivyo jambo ambalo liliinyima timu yake fursa ya kupata bao.

Hayo ni miongoni mwa makosa ya wazi ambayo yamekuwa yakijadiliwa zaidi juu ya mchezo huo uliochezwa Oktoba Mosi mwaka huu na kumalizika kwa matokeo ya sare ya bao 1-1.

Kutokana na kutoridhishwa na kiwango cha maamuzi yake, TFF iliamua kuwaondoa Saanya na Mpenzu katika orodha ya waamuzi wa Ligi Kuu na kisha kumkabidhi kwa Kamati ya Waamuzi ili waweze kushughulikiwa kitaalam zaidi ambapo tayari kamati hiyo imethibitisha kuwaondoa moja kwa moja katika orodha ya waamuzi wake.

Hata hivyo kumekuwa na sintofahamu kubwa kuwa kwanini imechukua muda mrefu kuwapa waamuzi hao adhabu wakati kamati ingeweza kutoa adhabu muda mfupi tu baada ya kufanyika kwa mchezo huo. Hakukuwa na ulazima wa kusubiri miezi miwili na zaidi ndipo kamati iweze kutoa adhabu.

Wazungu wana usemi wao mmoja unaosema ‘Justice delayed is justice denied’ wakimaanisha kuwa haki inayocheleweshwa ni sawa na haki inayonyimwa. Msimamo huu ndiyo umekuwa ukiwafanya Wazungu kuchukua maamuzi ya haraka hasa pindi jambo linapotokea na linakuwa na madhara makubwa.

Kutokana na msimamo huo tulipenda kuona adhabu kwa waamuzi zikitolewa pindi tu wanapofanya makosa ili kuziondolea timu nyingine uwezekano wa kukumbana na maamuzi mabovu ambayo yanatokana na Waamuzi hao.

Mfano tangu Oktoba Mosi Saanya alipodaiwa kuharibu mechi ya Simba na Yanga, amechezesha mechi nyingine tatu za Ligi Kuu jambo ambalo halikustahili.

Kama Mwamuzi ameharibu mechi kwa kiwango cha kuondolewa katika orodha ya waamuzi, kuendelea kumwacha achezeshe mechi nyingine ni kuhatarisha michezo hiyo.

Kama Kamati ya Masaa 72 iliweza kukaa na kufuta kadi nyekundu ya Jonas Mkude pamoja na kumfungia kwa miezi sita mwamuzi Ahmed Seif aliyekuwa amechezesha mechi ya African Lyon na Mbao FC chini ya kiwango, kulikuwa na haja pia ya kuwachukulia hatua Saanya na Mpenzu ili kuonyesha kuwa haki imetendeka.

Kusubiri miezi miwili na zaidi ili kutoa adhabu hiyo ni sawa na kuwaaminisha wapenzi wa soka kuwa kamati hiyo haifanyi kazi kwa utashi na weledi wa kutosha.

Kuna adhabu tangulizi ambazo zinaweza kutolewa kama vile kumsimamisha Mwamuzi ili kutoa nafasi ya kumchunguza kuliko kuendelea kumchunguza mtuhumiwa huku anaendelea na majukumu yake kama kawaida.

Kwa upande wa mwamuzi Rajab Mrope ambaye aliharibu mchezo wa Mbeya City na Yanga naye amepewa adhabu ambayo itamsaidia kupandisha kiwango chake lakini pia imetolewa kwa kuchelewa.

Ikumbukwe kuwa mechi hiyo ya Yanga na Mbeya City ilichezwa mwanzoni mwa Novemba hivyo adhabu hiyo imetolewa baada ya mwezi mmoja jambo ambalo si sahihi pia.

Mwamuzi anapoharibu mechi anatakiwa kuchukuliwa hatua ndani ya siku tatu kutokana na ukweli kwamba soka ni mchezo wa wazi na hakuna sababu ya kusubiri wiki nne ama tano ili kufanya maamuzi.

Adhabu kama hizi zinazotolewa kwa kuchelewa zinaishia kuibua maswali mengi badala ya kuonyesha kuwa watuhumiwa hao walikuwa na makosa na walistahili adhabu. Kama mwamuzi ameharibu mchezo anapaswa kuchukuliwa hatua mara moja.

Hiyo itasaidia kuondoa minong’ono kwa wapenzi wa soka ambayo inaweza kuchukua muda mrefu na na mara kadhaa inaweza kuathiri mwelekeo wa wale ambao wanapaswa kutoa adhabu kwa makosa husika.

Tungependa kuona Bodi ya Ligi na TFF zikifanya kazi kwa weledi zaidi na kuchukua hatua mara moja pindi kunapokuwa na makosa kwa upande wa waamuzi.