Bandari waitafutia dawa Sofapaka FC

Friday February 2 2018

 

By ABDULRAHMAN SHERIFF

MOMBASA. NI wakati wa hamu na ghamu kwa mashabiki wa soka wa Mkoa wa Pwani wakiomba timu yao ya pekee inayoshiriki Ligi Kuu ya Kenya, Bandari FC ipate ushindi katika mchuno wao wa ufunguzi wa ligi hiyo utakaochezwa Jumapili dhidi ya Sofapaka FC.

Mashabiki hao watakuwa wakifuatilizia kwa njia mbalimbali za mawasiliano kufahamu jinsi mechi hiyo itakayopepetwa uwanja wa Narok utakavyokuwa ukiendelea huku wakitia mnaombi maalum ya kuiombea timu yao hiyo imalize pambano hilo ikitia kibindoni pointi zote tatu.

“Nina imani kubwa vijana wangu watacheza soka la hali ya juu na wanatambua kuwa mashabiki wetu wanatarajia kupata ushindi ili tuanze ligi na motisha wa kufanya vyema kubeba taji ama kumaliza katika nafasi bora zaidi ya msimu uliopita,” alisem Kocha Mkuu Ken Odhiambo.

Akiongea wakati wa mazoezi ya mwisho ya timu hiyo kabla ya kuondoka jana kuelekea Narok, Odhiambo alisema ana matumaini makubwa ya timu kuanza kwa kupata ushindi.

“Kila kocha huenda vitani akiwa na tamaa kubwa ya kushinda vita hivyo na timu yangu ya Bandari inakwenda kupambana na Sofapaka nikiwa na matumaini ya kupata ushindi,” akasema mkufunzi huyo aliyechukua nafasi ya Paul Nkata aliyekamilisha mkataba wake na klabu hiyo.

Juu ya wanasoka watano waliokuwa wakiuguza majeraha, Odhimbo alisema itategemea umuzi wa wauguzi wa timu kusema kama wanaweza kuchezeshwa ama bado waendelee na matibabu. “Lakini wamefanya mazoezi na wanaonekana wako sawa,” akasema.