Azam wafalme Kombe la Mapinduzi

Saturday January 13 2018

 

By THOBIAS SEBASTIAN

Zanzibar. Azam imefanikiwa kutetea ubingwa wake wa Kombe la Mapinduzi baada ya kuifunga URA kwa penalty 4-3 katika mchezo wa fainali uliopigwa kwenye Uwanja wa Amaan, Zanzibar.

Kipa wa Azam, Razak Abalora alikuwa shujaa wa mchezo huo baada ya kuokoa penalti mbili za Patrick Mbowa na Brian Majwega pamoja na kuokoa hatari nyingi katika mchezo huo.

Kipa huyo raia wa Ghana alichaguliwa kuwa mchezaji bora wa mchezo huo ambao ulishuhudia kandanda safi ndani ya dakika 90.

Aggrey Morris ndiye aliyewapa shangwe vijana wenzake wa Chamazi baada ya kufunga penalti ya mwisho, akisahihisha makosa ya Bruce Kangwa aliyekosa penalti ya tatu na kupoteza uongozi wao.

Wachezaji wengine wa Azam waliofunga penalti zao ni nahodha, Himid Mao, Yakubu Mohammed na Enock Atta Agyei. Waliofunga kwa upande wa URA ni Sewa, Shafiq Kagimu na Jimmy Kulaba.

Kocha wa Azam Aristica Cioaba alisema katika mechi ya leo hataacha kumpa pongezi kipa wake Razack Abarola kwani anastahili kuwa mchezaji bora wa mashindano hayo.

"Lengo letu lilikuwa kuchukua ubingwa nashukuru Mungu tumefanikiwa hilo na tunawekeza nguvu katika mechi za ligi kuu ambayo  inayofaata tunacheza dhidi Ya Majimaji, " alisema Cioaba

Abarola alipanga penati mbili ambazo Patrick Mbowa na Brian Majegwa, Charlse Ssempa, Shafik Kagimu na Denis Kamanzi wakifunga.

Ndani ya dakika 90 za mchezo huo, timu zote mbili zilitengeneza nafasi za kufunga lakini washambuliaji wake hawakuwa na umakini wa kutosha katika kuzitumia ili kupata mabao.

Kipa wa Azam, Abalora alilazimika kufanya kazi ya ziada kuiweka timu yake mchezoni baada ya kupangua mashuti matatu ya maana katika kipindi cha pili. Kiwango chake katika mchezo huo ulimfanya achaguliwe kuwa mchezaji bora wa mechi.

Washambuliaji wa Azam, Bernard Athur, Iddi Kipagwile na Enock Agyei walipoteza nafasi za wazi katika mchezo huo katika kila kipindi jambo ambalo lilazimu mchezo kuamuliwa kwa mikwaju ya penalti ambayo ilimpa ushujaa Abalora.