Dodoma yachezea, JKT yanusa Ligi Kuu

Saturday January 13 2018

 

By CHARLES ABEL

Dar es Salaam. WAKATI mambo yakimwendea vibaya Jamhuri Kihwelo 'Julio', JKT Tanzania imetanguliza mguu mmoja ndani ya Ligi Kuu Bara msimu ujao baada ya kuifumua Mvuvumwa mabao 3-0 katika mfululizo wa mechi za Ligi Daraja la Kwanza (FDL).

JKT ilipata ushindi huo wa kishindo kwenye Uwanja wa Uhuru, jijini Dar es Salaam na kufikisha pointi 28 ikisaliwa na mechi tatu kabla ya kumaliza msimu, huku sasa ikihitaji pointi nn e tu kujihakikisha kupanda Ligi Kuu msimu ujao.

Ushindi huo umeifanya timu hiyo inayonolewa na Bakari Shime kujiimarisha kileleni, ikizidi kuzikacha Friends Rangers na African Lyon zilizopo nyuma yao na alama zao 19 na 18 ambazo leo zitapepetana katika mchezo mwingine mkali wa ligi hiyo.

Kwa kuangalia uwiano wa mabao na michezo iliyosalia ni kama vile JKT imeshapanda daraja isipokuwa inasubiri tu ratiba kuwaidhinisha mwishoni mwa msimu wa ligi yao, ingawa katika soka lolote linaweza kutokea.

Katika mechi nyingine ya ligi hiyo Dodoma FC ya Julio ilikumbana na kipigo cha mabao 2-0 ugenini mjini Tabora kutoka Rhino Rangers na kutibuliwa kasi yao ya kupanda daraja, hali iliyoikumba pia Alliance iliyolala mabao 2-0 kwa Biashara Mara.

Biashara imeishusha Dodoma FC kwani imefikisha pointi 23 dhidi ya 21 ya Vijana wa Julio, huku Alliance ikisalia nafasi ya tatu katika kundi hilo la C na alama zao 18.

Mjini Mbeya, wenyeji Mbeya Kwanza ilitoka suluhu na KMC, huku Mlale JKT ikishinda bao 1-0 dhidi ya Mawenzi Market wakati Coastal Union ikiishindilia Mufindi United kwa mabao 3-0 na Kiluvya United kulala 3-1 kwa Mgambo JKT ilihali  Toto Africans ililazimishwa suluhu nyumbani na JKT Oljoro.