Haiya! Cheki dili ya Kenyatta kwa Mashemeji

Saturday January 13 2018

 

By THOMAS MATIKO

Nairobi. AISEE! ngoma inazidi kushika. Nikwambie kitu? Sasa baada ya Sportpesa kuchorea udhamini wake sio tu kwa vilabu vya Gor Mahia na AFC Leopards, bali pili udhamini wa ligi kuu yenyewe, sasa serikali iliyoikazia maisha Sportpesa, imejibu mapigo kwa kupampu Sh50 milioni kudhamini msimu huu wa ligi 2018.

Taarifa za uhakika tulizozinasa Mwanaspoti ni kwamba, Wizara ya Michezo imeanzisha mikakati ya kuziba mapengo yote yaliyoachwa na Sportpesa iliyoondoa udhamini wake kwenye sketa zote za michezo nchini, baada ya serikali kushinda kesi iliyokuwa imewasilishwa na kampuni hiyo ya kubeti ikipinga sheria ya nyongeza ya kodi kwa asilimia 35 zaidi.

Na katika kufanya hilo, Wizara hiyo imetoa Sh50 milioni kwa ajili ya kugharamia mahitaji ya timu na kuendesha msimu mpya wa ligi kuu KPL mwaka huu utakaoanza mwezi ujao.

Lakini kando na hiyo, Wizara pia imesema itahakikisha kuwa Gor na AFC hazikosi kushiriki mechi zao za kimataifa za CAF, Champions League na Confederation mtawalia. Hivyo basi itagharamia safari zao zote za mechi za ugenini. Hatua hii imetoa ishara ya wazi kwamba, serikali haina nia kabisa ya kulegeza msimamo wake wa kupunguza sheria hiyo mpya ya makato ya kodi kwa kampuni za kubeti. Sportpesa walipojiondoa walikuwa na matumaini makubwa kwamba, hatua yao itatikisa sekta na hivyo kuishurutisha serikali kuingia mezani nao ili kuafikiana makubaliano ya kupunguza a kiwango hicho cha makato ya kodi.

Akifunguka, Katibu wa kudumu wa wizara hiyo Kirimi Kaberia ameichekea Sportpesa kwa kusema kujiondoa kwao hakujapunguza lolote. “Sportpesa wamejiondoa ndio ila hamna tatizo kabisa kwa sababu kuanzia sasa ni sisi ndio tutakaokuwa tukihusika kwenye dili zote za udhamini kati yetu na Mashirikisho,”  Kaberia ametupia dongo.

Kwa taarifa hiyo, Gor na AFC wamepata afueni kubwa kwani sasa wataweza kuelekeza nguvu zao katika kuhakikisha kuwa wanajitahidi kufika hatua ya makundi katika mashindano hayo ya kitaifa ambako ndiko kuna chapaa za uhakika.