Maoni ya Mhariri: Bila kujipanga vema ni ndoto kufika walipofika wenzetu

Tuesday October 10 2017

NIGERIA na Misri zimekuwa timu za kwanza kutoka Afrika kufuzu fainali za Kombe la Dunia za mwaka 2018. Tunazipongeza timu hizo kwa mafanikio hayo.

Ni mafanikio ambayo yamekuja baada ya timu hizo kupambana kwenye mechi zao makundi baada ya kuiacha Tanzania katika hatua mbili za awali za mbio hizo. Kwa wanaokumbuka katika mbio hizo za kuwania tiketi ya kwenda Russia, nchi itakayofanyikia fainali hizo za Dunia, Tanzania katika hatua ya awali kuliwang’oa Malawi na kupangwa kuvaana na Algeria.

Kila mmoja anakumbuka timu yetu, Taifa Stars ilivyokumbana na kiama mbele ya Mbweha hao wa Jangwani waliotufunga jumla ya mabao 9-2.

Wababe wetu hao walifuzu hatua ya tatu na ya mwisho ya kuisaka tiketi kwa kupangwa katika Kundi B lililotajwa kuwa la kifo sambamba na Nigeria, Zambia na Mabingwa wa Afrika Cameroon.

Ni vigumu kuamini kuwa Algeria na ubabe wake wote ndani ya kundi hilo ndio vibonde wakiburuza mkia wakiwa na pointi moja tu, baada ya kucheza mechi tano mpaka sasa wakiwa wamepoteza michezo nne, wakisaliwa na mechi moja. Inashangaza kidogo, lakini ndivyo soka lilivyo. Waliotuchapa mabao 7-0 baada ya sare ya 2-2 nyumbani, walikwenda kuwa wanyonge mbele ya wababe wenzao na hivyo kushindwa kwenda Russia katika fainali za mwakani.

Kwanini tumeamua kukumbushia safari ya Tanzania katika kuwania fainali hizo kwa kurejea mafanikio ya Nigeria na Misri kutangulia Russia?

Hii ni kwa sababu, imekuwa ni desturi kwa wadau wa soka hasa mashabiki kutamani mno kuona timu yao ya Tanzania ikifanikiwa kuingia kwenye historia ya kushiriki fainali kubwa, bila kujali maandalizi na mipango yetu ipoje.

Ni haki ya wadau kuota mafanikio hayo, lakini timu yetu na wachezaji wetu wameandaliwa kwa ajili ya ushindani wa kuwania tiketi za michuano mikubwa?

Mwanaspoti tunalisema hivi kwa kutambua kuwa baada ya kuondolewa katika mbio za kwenda Russia na fainali za Afrika kwa nyota wa ndani (CHAN 2018) tiketi pekee tuliyonayo ni tiketi ya Fainali za Afrika (Afcon 2019) za Cameroon.

Tupo kundi moja na nchi za Cape Verde, Lesotho na majirani zetu wa Uganda na tayari tumeshacheza mchezo mmoja nyumbani dhidi ya Lesotho na kuambulia pointi moja baada ya sare ya bao 1-1 Uwanja wa Chamazi, jijini Dar es Salaam.

Machi mwakani Stars itakuwa na kibarua cha kucheza na Uganda na Cape Verde mara mbili na kurudiana na Lesotho ugenini, ili kujua hatma ya Tanzania kama itaenda Cameroon ama la!

Ukipiga hesabu mpaka sasa ni kwamba Tanzania bado tuna kazi kubwa katika kuhakikisha tunaenda Cameroon, kwanza ni aina ya soka ambalo gtimu yetu imekuwa ikicheza kwa siku za karibuni.

Maandalizi yetu kwa ujumla bado yanaleta shaka na hasa kuamua kucheza mechi za kirafiki na timu laini tena mara zote nyumbani, lakini pia hakuna kikosi cha kwanza cha kueleweka kwa sasa ndani ya Stars.

Kila mara timu ikiitwa inakuwa na sura mpya, ukiacha wachache ambao ni tegemeo na hasa wanaocheza soka la kulipwa nje ya nchi.

Nini rai yetu? Ikiwa ni kweli tuna nia ya dhati ya kwenda katika fainali za aina yoyote, kwanza ni lazima tufanye maandalizi ya muda mrefu. Tusiwe watu wa kukurupuka na kuamini kuna miujiza itakayotubeba.

Cape Verde tulionao kundi moja, imefika ilipo kwa mipango mkakati na utekelezaji katika kuinua soka lao. Hata Misri inakwenda Russia baada ya miaka michache ya kupotea kwenye ufalme wa soka la Afrika. Ni wazi Wamisri walitambua kwanza tatizo lao, wakalikalia chini na kulitatua na sasa wanakula matunda kwa kurejea katika fainali za dunia baada ya kuzikosa kwa zaidi ya miaka 20 tangu walishiriki mara ya mwisho 1990 fainali zilizochezwa Italia.

Hata katika soka la Afrika, Misri ilipotea baada ya kuzikosa fainali za Afcon tangu iliposhiriki na kubeba taji lao la mwisho mwaka 2010 kabla ya kuibuka mwaka huu iliposhika nafasi ya pili nyuma ya mabingwa Cameroon.

Hii ni kuonyesha hatuwezi kufika kokote kwa mipango ya zimamoto au ndoto za alinacha, wadau lazima wakubali kuwa mafanikio ya kitu chochote yanakuja kwa mipango madhubuti na maandalizi ya kutosha tangu awali, si kwa staili yetu hii.