Tshishimbi atua Pemba kwa kishindo tayari kuivaa Simba

Pemba. Kiungo wa mpya wa Yanga, Papy Tshishimbi amewasili kisiwani Pemba tayari kuungana na kikosi hicho kinachojiandaa na mechi dhidi ya Simba itakayochezwa Jumatano ijayo kwenye Uwanja wa Taifa Dar es Salaam.

Papy aliwasili Pemba  saa 9:27 alasiri kwenye Uwanja wa Ndege wa Pemba na kupokelewa na meneja wa kikosi hicho Hafidh Saleh.

Akizungumza  baada ya kuwasili Papy alisema ilikuwa afike mapema kujiunga na timu yake hiyo, lakini kikubwa kilichomzuia ni kuchelewa kwa pasi yake mpya ya kusafiria ambayo ilichelewa kutoka baada ya ile ya awali kuwa katika hatua za mwisho kumalizika.

Papy alisema pamoja na kuchelewa hajafanikiwa kuipata pasi hiyo kutokana na kulazimika kuwahi kujiunga na wenzake kujiandaa na mechi dhidi ya Simba.

Kiungo huyo anayetua Yanga akitokea Mbambane Swallows ya Swaziland alisema anahitaji kujifua kwa siku chache kuweka mwili.

Haikuwa kazi rahisi kwake kuondoka Mbambane kutokana na klabu hiyo bado inamuhitaji na kuwalazimu baadhi ya marafiki na mashabiki kulia na kuwapigia makelele viongozi wa klabu yake, lakini aliamua yeye binafsi kutaka kubadili maisha kwa kuhamia klabu nyingine.

"Nimefurahi sana kuwa hapa, nimekuja kuitumikia Yanga naamini nitafanya kazi ambayo mashabiki wa Yanga wataifurahia nimeambiwa walikuwa wananisubiri,"alisema Papy.