Simba wapewa Bil 4 wagawane

Muktasari:

Wanachama hai wa Wekundu wa Msimbazi wameangukiwa na neema hiyo ambapo sasa watapewa hisa zenye thamani ya Sh4 bilioni wagawane, ikiwa ni ujira wao kwa kuitumikia timu hiyo ya Msimbazi kwa muda mrefu.

WANACHAMA wa Simba wana kila sababu ya kuchekelea mabadiliko mapya ya mfumo wa uendeshaji wa klabu yao, hiyo ni baada ya neema nzito kuwaangukia.
Wanachama hai wa Wekundu wa Msimbazi wameangukiwa na neema hiyo ambapo sasa watapewa hisa zenye thamani ya Sh4 bilioni wagawane, ikiwa ni ujira wao kwa kuitumikia timu hiyo ya Msimbazi kwa muda mrefu.
Juzi Jumapili, bilionea Mohammed ‘MO’ Dewji alitangazwa kuwa mshindi wa zabuni ya kuwekeza klabuni hapo ambapo atachukua asilimia 50 ya hisa kwa Sh20 bilioni, japo serikali imesisitiza kwamba mwekezaji hapaswi kuwa na zaidi ya asilimia 49 ya hisa za klabu.
Kwa mujibu wa mapendekezo ya mgawo wa hisa hizo, wanachama wanapewa asilimia 10
ambazo watagawana. Hisa hizo zina thamani ya Sh4 bilioni. Hisa nyingine asilimia 40 zenye thamani ya Sh16 bilioni zinabaki kama akiba kwa ajili ya kuuzwa baadaye.
Mjumbe wa Kamati ya Mabadiliko Simba, Mulamu Nghambi, alisema watahakiki wa wanachama kuwafahamu wanaostahili kupata mgawo. “Unajua kuna wengine hawajalipa ada zao kwa muda mrefu, Katiba inasema asiyelipa kwa miezi sita mfululizo amekoma
uanachama, tutawafahamu walio hai,” alisema.