Kumbe tatizo ni fungu la Yanga

MOHAMMED DEWJI: Mfadhili ambaye amekuwa akimwaga fedha ndani ya Simba kabla ya kuibuka kutaka alipwe chake Sh1.4 bil.

Muktasari:

  • Mara baada ya kusainiwa mkataba huo, juzi Jumapili vigogo wa Simba akiwemo Zacharia Hanspoppe pamoja na mfadhili wa klabu hiyo, Mohammed Dewji ‘MO’ walitangaza kubwaga manyanga kwa maelezo kwamba hawakuhusishwa kwenye dili hilo.

KASHESHE kubwa linaendelea ndani ya Simba chanzo kikiwa ni mkataba mpya waliosaini na kampuni ya SportPesa ya Kenya, lakini uchunguzi wa Mwanaspoti jana Jumatatu umebaini tatizo jipya.

Simba ilisaini mkataba huo wa miaka mitano Ijumaa iliyopita ukiwa na thamani ya Sh4.96 bilioni ambapo kwa mwaka watakuwa wanachukua Sh888 milioni pamoja na bonasi mbalimbali ambazo zitatokana na ufanisi wao kwenye mashindano ya ndani na nje ya nchi.

Mara baada ya kusainiwa mkataba huo, juzi Jumapili vigogo wa Simba akiwemo Zacharia Hanspoppe pamoja na mfadhili wa klabu hiyo, Mohammed Dewji ‘MO’ walitangaza kubwaga manyanga kwa maelezo kwamba hawakuhusishwa kwenye dili hilo.

Lakini si hao tu, hata baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Utendaji nao wako kwenye hatihati ya kujiondoa kwa maelezo kwamba walionyeshwa baadhi ya vipengele vya mkataba huo siku moja kabla ya kusainiwa kwake, jambo ambalo wamedai ni kinyume na utaratibu wao wa kuendesha mambo.

Pamoja na hayo yote, lakini uchunguzi wa Mwanaspoti ambayo ilikutana chemba na wajumbe kadhaa wa Simba juzi na jana ulibaini kuwa wamegundua kitu kwenye dili la Yanga na SportPesa.

Habari zinasema kwamba wajumbe hao wamefanya uchunguzi wao na kubaini kuwa Mwenyekiti wa Yanga, Yusuf Manji amewakomalia SportPesa wakaipa Yanga dau kubwa kuliko wao. Habari zinasema kuwa Simba wamebaini Yanga itapewa dau la Sh950 milioni kwa mwaka tofauti na Mnyama ambaye Evans Aveva amesaini mkataba wa Sh888 milioni kwa mwaka.

Hiyo inamaanisha kwamba Yanga watalamba zaidi ya Sh5 bilioni kwa miaka mitano.

Ingawa SportPesa jana hawakuwa tayari kutoa ufafanuzi wa kina kuhusu na hilo, lakini habari zinasema kwamba walipanga kusaini mkataba na Yanga leo Jumanne kwenye makao makuu pale Jangwani,  lakini wameahirisha kwasababu ambazo hatahivyo hazijawekwa wazi.

Habari zinasema kwamba Simba wamebaini kwamba Manji alikuwa anagoma kutoa nembo yake ya Quality Group kifuani mwa jezi kwenda begani mpaka walipolazimika kuongeza fungu hilo ambalo Simba wanadai wamelishtukia.

Wajumbe hao wa Simba wanadai kwamba MO alikuwa ameshafikia makubaliano na Acacia ambao walikuwa wasaini pale tu alipokuwa anaingia Simba kwa hisa asilimia 51. Wanadai kwamba Acacia walikuwa waipe Simba Sh2 bilioni kwa mwaka na nembo yao ikae kifuani ambapo sasa haiwezekani tena baada Aveva kusaini dili ya miaka mitano na SportPesa.

VIKAO HAVIISHI

Mwanaspoti linafahamu kwamba viongozi wa Simba kupitia Kamati ya Utendaji juzi Jumapili walikutana katika kikao cha dharura baada ya Hanspoppe kutangaza kujiuzulu na MO kutaka fedha zake alizoikopesha klabu hiyo ambazo ni Sh1.4 bilioni.

Habari kutoka ndani ya kikao hicho ambacho kilikuwa na mvutano kiasi, zilidai kikao kilimalizika usiku wa saa 9 ya kuamkia jana Jumatatu na kwamba  kilimshirikisha pia Hanspoppe ambapo alielezwa mchakato mzima ulivyokuwa hadi kufikia makubaliano hayo na Sportpesa ingawa vikao vya awali na kampuni hiyo alihudhuria.

“Tatizo ni kwamba Hanspoppe kikao cha mwisho kilichomaliza kila kitu hakuwepo kwani alisafiri, ila vikao vya mwanzo na Sportpesa alihudhulia, tumekutana jana (juzi) kikao kilikuwa kirefu sana, tumejadili na ameelewa nini kusudio letu ndiyo maana amebatilisha maamuzi yake ya kujiuzuru na hakuna kiongozi atakayejiuzulu sasa,” kilisema chanzo chetu.

“Unajua Wanasimba wanatakiwa waelewe hakukuwa na namna Simba ilipaswa kukubali udhamini huu kwa vyovyote sababu kubwa ni moja, mchakato wa uwekezaji wa MO bado ulikuwa hauna uhakika wa kukamilika, sasa hapo hapo tayari mhusika alishatueleza kwamba mpaka kufikia Mei sasa hataweza kutupa fedha zozote, sasa klabu itaendeshwaje? Ndiyo maana tukaamua kuingia mkataba.

“Nani anajua, hatujui hatima ya kesho kwa maana ya kwamba ligi itakapoanza kwani mchakato wa mabadiliko ya mfumo wa uendeshaji haujakamilika, ndiyo sababu kubwa ya sisi kukubali mkataba huo na yeye (MO) haijulikani kama angeendelea kuipa pesa Simba.”

HANSPOPPE AREJEA

“Hanspoppe baada ya kueleweshwa kilichofanyika, aliamua kufuta maamuzi yake ya kujiuzulu Simba na tunaendelea kuzungumza na MO Dewji,” alisema Makamu wa Rais wa Simba, Geofrey Nyange ‘Kaburu’ alipozungumza na Mwanaspoti.

“Nilisema tangu juzi kwamba kama kuna mtu anaona kuna mambo hayako sawa uongozi wa Simba upo tukutane na kuyaweka sawa hakuna haja ya kutupiana maneno wala kuchukua maamuzi ya jazba,tukifanya hivyo tutakuwa hatuisadii Simba.

“Kuhusu MO niseme tu uongozi wetu tunamheshimu na kwa sasa tumeshaanza kufanya taratibu za kukutana naye, tukae atueleze maoni yake lakini pia kama viongozi tutaongea na kumpa majibu katika mambo ambayo atatueleza, hatujajua tutampata lini kwasababu itategemea na upatikanaji wake kulingana na ratiba yake, lakini tambueni Simba ipo salama.

“Nitumie nafasi hii kuwaondoa wasiwasi wanachama  wetu watulie uongozi wao uko makini na tuko pamoja hakuna matatizo na akili yetu sasa ni kuangalia tunamalizaje ligi katika mechi moja iliyosalia na mchezo wa fainali ya FA kwa masilahi ya klabu yetu.”

MSIKIE KILOMONI

Lakini jana Jumatatu Mwenyekiti wa Baraza la Wadhamini wa klabu hiyo, Hamisi Kilomoni, aliibuka na kusema kuwa mfanyabiashara huyo hana chake Msimbazi.

Kilomoni anasema MO amejiingiza mkenge mwenyewe kwa kusaini makubaliano hayo na kutoa fedha Simba ikiwamo kulipa mishahara ya wachezaji wa timu hiyo.

Makubaliano hayo yanadaiwa yangesitishwa mwishoni mwa mwezi  huu, lakini ghafla akashtukiza mabosi wa Simba wamesaini dili ya SportPesa na kumchanganya.

Kilomoni anasema walitoa tahadhari hiyo baada ya kuona harakati za mabadiliko ya uendeshaji wa klabu, ili asubiri kwanza mpaka mchakato huo utakapokamilika.

“Kwani MO ashirikishwe kwenye mambo ya klabu kuingia kusaini mikataba na kampuni zingine zinazodhamini Simba akiwa kama nani? Binafsi sioni sababu ya MO kushirikishwa kwani si mfadhili wa klabu. Baraza la Wadhamini tulikutana na MO kama mara mbili kujadili mchakato huo ambao bado haujakamilika hadi sasa,” alisema Kilomoni.

“Tulichomwelekeza MO kukifanya ni kwamba aandike mapendekezo ya uwekezaji alioutaka kuufanya nakumbuka tumekuatna naye mara mbili tofauti, ila hajafanya hivyo mpaka sasa, mbali na hilo tulimshauri asisaini nyaraka yoyote na hawa viongozi  likiwemo pia suala la kutoa fedha zake mpaka tushirikishwe baraza la wadhamini. Tunashangaa hayo yote ameyakiuka na kufanya kinyume sasa anaibuka na kusema anadai sasa anayemdai nani?

“Hizo fedha ni vyema akawadai viongozi aliowapa na si klabu ya Simba kwa sababu mpaka uwe mkopo wa klabu ya Simba wenye mali ambao ni Baraza la Wadhamini tulipaswa kushirikishwa, sasa hivi hawezi kuja kuidai Simba kwa kuwa hatukuwa sehemu ya ushirikishwaji wa kutolewa kwa fedha hizo, sasa ni jinsi gani atalipwa deni lake hilo watajuana na viongozi ambao alikubaliana nao, hivyo MO anapaswa kuwa mtulivu kwa kipindi hiki.

“Ukiniambia Simba haina fedha binafsi siwezi kukuelewa, tuna majengo mawili ambayo yanaingiza fedha nyingi achana na hivi vyanzo vingine, Simba ilianzishwa na watu kwa kutoa pesa zao za mfukoni hivyo haiwezi kuendeshwa kama klabu ya mtu mmoja.”

MOGELLA ATAHADHARISHA

Naye straika wa zamani wa Simba, Zamoyoni Mogella, amekielezea kitendo cha Rais wa timu hiyo, Evans Aveva, kusaini mkataba na SportPesa ukingoni mwa msimu ndio chanzo cha tatizo la mtafaruku ambao  lazima utatuliwe mapema.

“Mkataba kama huo ulitakiwa kusainiwa baada ya kumalizika kwa msimu, ungezingatia kushirikisha Baraza la Wadhamini na ungekuwa wa wazi bila kuficha ficha mambo kama wanavyofanya, huo ni uroho wa pesa,” alisema Mogella.

“Hapo ndipo utajua mpira unaongozwa na wapiga dili na siyo wenye malengo ya kuleta maendeleo, watu wa kwanza kulaumiwa ni wale wanachama ambao wanakurupuka kuwachagua watu wasio na weledi wa kazi.

“Bundi ameshatua Msimbazi dalili yake mbele kuna kilio na wakisalimika mbele ya Mbao (katika fainali ya Kombe la FA)  ni bahati, viongozi wanaweza kuanza kujikita na migogogro badala ya kumaliza kwa mafanikio.”

RAGE AWATULIZA SIMBA

Mwenyekiti wa zamani wa Simba ambaye ana ushawishi mkubwa kwa wanachama na mashabiki wa klabu hiyo, Ismail Aden Rage, amewataka viongozi wa Simba kukaa pamoja na MO na Hanspoppe ili kuweka mambo sawa.

“Nilikuwa nawasihi wafanye uungwana na kukaa pamoja na MO na Hanspoppe ili kupunguza munkari kwa maslahi ya Simba. Waweke masilahi ya klabu mbele badala ya maslahi yao,” alisema Rage.

“Michezo iliyobaki kwa Simba ni muhimu mno na kunahitajika umoja na mshikamano, MO apunguze hasira na Hans kadhalika na kama ameamua kufuta msimamo wa kujiuzulu ni jambo zuri.

“Kama kuna tatizo walimalize sasa ama kujadiliana kwa kina baada ya kumalizika  msimu, wasiwavuruge wachezaji katika mechi hizo zinazoweza kuwapa ubingwa na tiketi ya michuano ya kimataifa.”