Mfaransa Simba ataja mechi za ubingwa

Muktasari:

  • Djuma alisema alikaa na bosi wake, Pierre Lechantre na walikubaliana kuwa wanatakiwa kufanya kila mbinu ili kushinda mechi hizo.

VINARA wa Ligi Kuu Bara, Simba, keshokutwa Jumapili watacheza mechi ya kimataifa dhidi ya Gendarmerie ya Djibouti, lakini huko kwenye Ligi Kuu Bara ni kama wamemaliza mambo kwani wenyewe wanasema kuna mechi saba tu ambazo wakishinda, ubingwa utakuwa umekamilika.

Kocha Msaidizi wa timu hiyo, Masoud Djuma,  amesema benchi la ufundi limejidhatiti kwa ajili ya mchezo wa keshokutwa lakini wameshapiga hesabu ya mechi hizo saba zijazo za ligi kuhakikisha wanashinda zote ili kujiweka katika mazingira salama ya kuchukua ubingwa.

Djuma alisema alikaa na bosi wake, Pierre Lechantre na walikubaliana kuwa wanatakiwa kufanya kila mbinu ili kushinda mechi hizo.

“Tumewekeza akili zetu, nguvu na maisha yetu yote msimu huu ili kuchukua ubingwa ambao ndio nafasi pekee iliyobaki kwetu kufanya vizuri na kupata nafasi ya kushiriki michuano ya kimataifa msimu ujao,” alisema.

“Kwa hiyo, tulikubaliana na Lechantre kuwa lazima tushinde mechi zetu saba zinazokuja bila kujali tunacheza nyumbani au ugenini, lakini tunatakiwa kuzifunga pia timu zote ambazo zipo katika Tano Bora kwenye msimamo wa ligi kuu.”

OKWI ASHINDIKANA

Wakati huo huo, kama ulikuwa unadhani ni kazi rahisi kumkaba staa wa Simba, Emmanuel Okwi, ambaye amefunga mabao 13 hadi sasa msimu huu, basi sahau kwani Azam wenyewe wamekiri kuwa walijipanga vilivyo, lakini staa huyo akawazidi maarifa.

Okwi aliifungia Simba bao pekee la ushindi walipoichapa Azam FC 1-0 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam juzi Jumatano hivyo kujitanua kileleni kwa pointi 41, saba zaidi ya wapinzani wao Yanga walio  nafasi ya pili.

Kocha Msaidizi wa Azam, Iddi Cheche, alisema walifanya maandalizi mazuri ya kumzui Okwi kwani ndiye mchezaji hatari zaidi katika safu ya ushambuliaji ya Simba, lakini walijikuta wanafanya kosa moja na Mganda huyo akalitumia hilo hilo kuwaadhibu.

Cheche alisema kila wanapocheza mechi yoyote ile lazima waangalie kuwa kuna mchezaji gani hatari ambaye anaweza kuwaletea madhara na kuandaa mikakati za kumzuia.

“Okwi ameonyesha kuwa ni mchezaji timamu na mkamilifu kwani tulikuwa tumepanga mikakati madhubuti ya kumzuia  asiweze kuleta hatari yoyote kwetu, lakini kosa moja tu ndani ya dakika 90 walilofanya mabeki wangu alilitumia kutuadhibu,” alisema Cheche.

“Ni mchezaji mjanja hivi na inatakiwa kumkaba kwa umakini usiooungua hata sekunde moja.”